Habari Mseto

Maafisa Ethiopia waomba usaidizi kuelewa taarifa za kisanduku

March 14th, 2019 2 min read

PHYLISS MUSASIA na AFP

MAAFISA nchini Ethiopia walisema JumatanoNdege:Maafisa wataka usaidizi kuelewa taarifa kuwa wameshindwa kusoma maelezo kwenye kisanduku cheusi kinachorekodi taarifa kwenye ndege.

Hapa nchini, familia zilizopoteza watu 32 kwenye mkasa wa ndege Jumapili, leo zinatarajiwa kwenda nchini Ethiopia kutazama miili.

Ziara hiyo iliyofadhiliwa na serikali, inafanywa huku katika kaunti ya Nakuru, familia iliyopoteza watu watano ikieleza pengo lililoachwa na binti yao, ambaye alikuwa tegemeo.

Bw John Quindos Karanja, anatarajia kuandamana na mwanawe kifungua mimba, Quindos Mwangi pamoja na kijana mkwe, Bw Paul Kihika hadi Addis Ababa.

Bw Karanja alimpoteza bintiye mkubwa Carolyne Karanja pamoja na mkewe Bi Ann Wangui Quindos na wanawe watatu Ryan Njoroge 7, Kelly Paul 5, na Ruby Paul wa umri wa miezi 9, walipokuwa safarini kutoka nchini Canada.

Jana, familia ilikumbuka jinsi Carolyne alivyokuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba wanakula na kuvalia vizuri, karo yao shuleni inalipwa kwa wakati na kwamba hawakosi lolote.

Huku machozi yakimlengalenga machoni, Kevin alielezea jinsi dadake alimwokoa alipokuwa akisomea udaktari nchini Venezuela.

Alisema alipata nafasi kwenda Venezuela kwa muda wa miaka saba kupitia uhisani wa serikali ya Kenya lakini serikali ilipomtema baadaye na nusura akose kufanya mtihani wake wa mwisho, Carolyne aliingilia kati na kulipa karo aliyodaiwa.

“Siwezi kuelezea ni vipi nitahisi bila dadangu mpendwa, amekuwa msaada mkubwa kwangu. Sikumuona tu kama dada ila pia rafiki wangu wa karibu kwani tuliweka naye siri nyingi,” akaelezea.

Serikali ya Ethiopia ilisema italazimika kupeleka kisunduku cha kunakili mawasiliano ya ndege katika mataifa ya Ulaya, huku ulimwengu ukitaka kujua kilichosababisha ajali hiyo iliyoua watu wote 157.

Ajali hiyo ni ya pili mbaya zaidi inayohusisha aina ya ndege ya Max -8 na imetokea katika kipindi cha miezi sita baada ya ile iliyohusisha ndege ya Indonesia.

Rais Donald Trump wa Amerika, ametilia shaka uwezo wa marubani kuendesha ndege za kisasa.

Akizungumza siku mbili baada ya ajali hiyo ya ndege, rais huyo mbishi alisema ndege zimekuwa ngumu zaidi kuendesha, na hivyo zinahitaji wataalamu wa teknolojia za kisasa zaidi kuliko marubani.

Alisema hayo huku serikali ya Amerika ikitetea usalama wa ndege za Boeing 737 MAX 8, nayo mataifa zaidi yakipiga marufuku utumizi wa ndege hizo baada ya ajali iliyosababisha vifo vya watu 157 Jumapili.

Uingereza, Australia, Malaysia, Singapore, Australia, Afrika Kusini, Brazil na Mexico zilijiunga na mataifa ambayo yalizuia utumizi wa ndege hizo huku ikiripotiwa marubani Argentina walisusia kuziendesha wakihofia usalama wao.

Lakini Mamlaka ya Kitaifa ya Ndege nchini Amerika (FAA) ilituma taarifa kimataifa kuhakikisha usalama wa ndege hizo.

Imefichuka pia kampuni hiyo imekuwa ikiendeleza mikakati ya kutengeneza upya miongozo ya mafunzo kwa marubani.