Maafisa wa DCI wakita kambi Kilifi kupeleleza serikali ya Kingi

Maafisa wa DCI wakita kambi Kilifi kupeleleza serikali ya Kingi

Na MAUREEN ONGALA

MAAFISA mbalimbali katika serikali ya Kaunti ya Kilifi wameingiwa na uoga baada ya maafisa wa idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutoka makao makuu jijini Nairobi, kupiga kambi katika kaunti hiyo.

Maafisa hao waliwasili katika afisi za katibu wa Kaunti ya Kilifi Bw Arnold Mkare, Jumatatu asubuhi wakafanya uchunguzi kuhusu ufisadi kwa siku mbili mfululizo.

Akizungumza afisini mwake mjini Kilifi, Bw Mkare alisema uchunguzi ulihusu masuala ambayo yalikuwa yanapelelezwa tangu kitambo.

“Tumekutana nao na kuzungumza nao kuhusu masuala wanayofuatilia ikiwemo stakabadhi mbalimbali ambazo walikuwa wanahitaji kutoka katika idara zetu,” akasema.

Hata hivyo Bw Mkare alikana madai kuwa kuna baadhi ya maafisa wa kaunti ambao wametiwa mbaroni.

Alisema baadhi ya stakabadhi wanazohitaji zinahusu jengo jipya la matibabu la mamilioni ya pesa lilanojenjwa katika Hospitali ya Kaunti ya Kilifi.

Sehemu ya jumba hilo linatumika kwa kuwahudumia wagonjwa mahututi wa Covid-19.Aliongeza kusema kuwa maafisa hao pia walikuwa wanafuatilia maafisa wengine wa kaunti ambao walihitajika kuandika taarifa zao.

“Kuna baadhi ya maafisa kutoka idara tofauti ambao walihitajika kufika katika afisi za upelezi wa jinai Nairobi mwaka 2020. Kunao pia baadhi ambao hawakwenda na imebidi maafisa hao wa upelelezi kuwafuatlia ili kunakili taarifa zao,” akasema Bw Mkare.

Baadhi ya maafisa wa kaunti ambao walienda Nairobi ni Afisa Mkuu wa wizara ya barabara Bw Ken Kazungu na mkurugenzi wa maswala ya maji Bi Mapenzi Chivila.

Afisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa alisema majasusi wanachunguza nakala zote za miradi kuanzia mwaka wa 2014.

“Kila mfanyakazi yuko roho mkononi kwani hatujui ni nani atakayetiwa mbaroni na maafisa hawa,” akasema.

Jumanne mchana, msafara was magari matatu, moja likiwemo la Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) yalikuwa yanatoka katika ofisi za katibu wa kaunti. Gari moja lilikuwa limewabeba maafisa kadha wa serikali ya kaunti.

Magari hayo yalielekea katika ofisi kuu za upelezi mjini Kilifi.

Afisa mkuu wa upelezi Kaunti ya Kilifi, Bw Geoffrey Kathurima alithibitisha uchunguzi unaoendelea.

“Ninaufahamu kuwa maafisa hao wanafatilia kesi ambazo tayari uchunguzi unaendelea, wako hapa kufanya kazi yao,” akasema.

Mwezi Mei mwaka jana, maafisa kutoka EACC waliwatia mbaroni Katibu Mkuu wa Kaunti ya Kilifi Bw Arnild Mkare, Afisa Mkuu wa matibabu Bw Bilal Mazoya na mwenzake wa afya ya umma Bw Bilal Madzoya kwa madai kuwa walikataa kupena habari muhimu za kusaidia katika upelezi wa kesi tofauti katika kaunti hiyo.

Maafisa hao wakuu walilaumiwa kwa kukosa kupatiana nakala kuhusu mradi wa jengo la matibabu lilokuwa linaendelea kujengwa.

You can share this post!

Ngoma ya BBI itarindima tena – Joho

Ni rasmi kuwa Martha Koome ndiye Jaji Mkuu wa Kenya