Maafisa wa KDF wahofiwa kuuawa kwa bomu Lamu

Maafisa wa KDF wahofiwa kuuawa kwa bomu Lamu

Na KALUME KAZUNGU

WANAJESHI kadhaa wa kikosi cha KDF wanahofiwa kufariki na wengine kujeruhiwa, baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa barabarani katika eneo la Baure, Lamu Mashariki.

Wanajeshi hao walikuwa wakisafiri kwa gari la kupiga doria wakati mkasa huo ulipotokea jana mwendo wa saa tatu unusu asubuhi.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia alithibitisha mkasa huo unaoshukiwa ulitekelezwa na wapiganaji wa kundi la al-Shabaab.

Mkasa ulitokea siku mbili tu kabla Rais Uhuru Kenyatta kuzuru Kaunti ya Lamu kwa mapokezi ya meli ya kwanza inayotarajiwa kutia nanga katika bandari mpya hapo kesho.

Hata hivyo, kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hii, idadi halisi ya wanajeshi waliokuwa katika msafara huo ilikuwa haijajulikana.

Bw Macharia alisema thibitisho kuhusu idadi ilichelewa kwa vile eneo ambapo mkasa ulitokea ni mbali.

Eneo la Baure liko ndani ya Msitu wa Boni, ambapo serikali kuu imekuwa ikiendeleza oparesheni ya “Linda Boni” kupambana na magaidi tangu 2015.

Oparesheni hiyo hulenga kuondoa magaidi wa kundi la al-Shabaab wanaoaminika wamejificha msituni.

Bw Macharia alisema maafisa wa usalama wameanzisha msako mkali eneo hilo na akawaomba Wakenya wasiwe na hofu wala kutishika.

“Kwa sasa sina habari za kutosha. Ninasikia kulikuwa na shambulio kutoka kwa maadui mapema asubuhi. Bado hatujafanikiwa kubata habari kamili kwa sababu mawimbi ya mawasiliano ni mabaya. Inawezekana kuna vifo na majeruhi lakini hakuna sababu ya kuhofia. Bado tuko imara,” akasema.

Duru kutoka kwa idara ya polisi zilisema kikosi cha KDF kilichokuwa kikipiga doria asubuhi kilikanyaga bomu la kujitengenezea ambalo lilitegwa barabarani Baure, na kusababisha wanajeshi kadhaa kupoteza maisha yao na wengine wakajeruhiwa.

“Kuna wanajeshi ambao walifariki katika kisa hicho. Adui analenga vyombo vya usafiri vya kupiga doria,” akasema afisa aliyeomba kutotajwa kwa vile hana mamlaka kuzungumzia suala hilo kwa wanahabari.

Kisa hicho kilitokea wiki mbili tu baada ya watu wawili kuuawa na mmoja kujeruhiwa vibaya wakati gari ambalo walikuwa wakitumia kusafiri lilipokanyaga bomu barabarani katika mpaka wa Lamu na Somalia.

Mnamo Machi 23, mtu mmoja alifariki wakati lori la kusafirisha maji kuelekea kambi ya Usalama, ambapo ukuta wa mpaka wa Kenya na Somalia unajengwa, lilipokanyaga bomu mwendo wa saa moja unusu usiku.

You can share this post!

Oimeke wa ODM aibuka mshindi wa kiti cha ubunge Bonchari

BBI: Serikali yaandaa rufaa ya uamuzi