Habari Mseto

Maafisa wa Kenya Power mashakani kuhusu kupotea kwa ushahidi

October 24th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

SIKU moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuungama mahakamani kuwa nakala muhimu za ushahidi katika kesi ya ununuzi wa transfoma mbovu zimeibwa aliyekuwa wakili na katibu wa kampuni ya Kenya Power (KP) Beatrice Meso na washukiwa wengine wawili walikamatwa na kufikishwa kortini Jumanne.

Bi Meso , Bw John Muchere Ombui na Bi Ruth Oyile walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot na kuombwa aamuru wazuiliwe kwa muda wa siku saba na Polisi kuwasaidia katika uchunguzi.

“Naomba hii mahakama iwazuilie washukiwa hawa watatu katika kituo cha Polisi cha Muthaiga kwa muda wa siku saba,” alirai kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi.

Mbali na kuzuiliwa kwa muda huo, Bi Nyamosi aliomba washukiwa hao wasikubaliwa kujibu mashtaka kadhaa waliyofunguliwa kuhusiana na kutoweka kwa ushahidi huo muhimu katika kesi dhidi ya waliokuwa wakuu wa kampuni ya KP Dkt Ben Chumo , Dkt Ken Tarus na washtakiwa wengine 13.

“Naomba hii mahakama isiwasomee washukiwa mashtaka dhidi yao hadi Polisi wakamilishe uchunguzi walioanza kusaka nakala za ushahidi uliopotea kabla ya kuanza kwa kesi dhidi ya Dkt Chumo na wengine,” alisema Bi Nyamosi.

Kiongozi huyo wa mashtaka alimsihi hakimu akubalie ombi la  DPP kwamba washukiwa hao wazuiliwe kwa muda wa siku saba kusaidia polisi kukamilisha uchunguzi.