Habari Mseto

Maafisa wa KRA wanasa katoni kadha za pombe

November 15th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MAAFISA wa KRA kutoka jijini Nairobi wamenasa katoni kadha za pombe chapa ya Vodka.

Wakiongozwa na afisa wa KRA Bi Anne Irungu, maafisa hao walizuru kijiji cha Kiandutu, mjini Thika na kunasa katoni 198 zilizokuwa zimepakiwa kwa gari moja.

“Maafisa wa MultiAgency ndio waliofanya juhudi kuinasa pombe hiyo haramu katika kijiji cha Kiandutu huku wakishuku kuwa haikuwa imelipiwa ushuru inavyostahili,” alisema Bi Irungu.

Alisema wataendelea kufanya uchunguzi zaidi kubaini iwapo pombe hiyo imelipiwa ushuru inavyostahili na pia kama imebandikwa alama halali za KRA katika chupa hizo za pombe.

“Iwapo tutagundua ya kwamba mwenye pombe hiyo hakufuata sheria inayostahili, bila shaka atafunguliwa mashtaka mara moja na kufikishwa mahakamani,” alisema afisa huyo wa KRA.

Alisema tayari mshukiwa mmoja ametiwa nguvuni ambapo anaendelea kuhojiwa huku akitarajia kufikishwa mahakamani mara moja.

Afisa wa KRA Bi Anne Irungu akihutubia waandishi wa habari mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Aliwataka wanywaji wa pombe kuwa makini wakati wanaikunywa pombe kwa kuhakikisha kuna alama maalum ya KRA ya ‘Soma Label’ ambayo limebandikwa katika chupa za pombe.

Alisema walinasa katoni 198 ambapo zimekosa kulipiwa ushuru wa takribani Sh1 milioni.

Alisema tayari maafisa wa KRA wanaendelea kufanya msako mkali katika maeneo muhimu ili kunasa wamiliki wa biashara ya pombe ambao hawajalipia ushuru.

Alisema kampeni yao sasa inalenga mashinani kwa sababu huko ndiko watu wengi wanabugia pombe kwa viwango vya juu.

“Hatutaki kuona wananchi wakiuziwa bidhaa hatari kwa afya zao, na kwa hivyo wale wanaoendelea kuuza pombe haramu wajue siku zao zimewadia na watakumbana na sheria vilivyo,” alisema Bi Irungu.