Kimataifa

Maafisa wa mbuga wadai Sh1.9 milioni zilizopotea zilimezwa na sokwe

July 24th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

POLISI nchini Nigeria wanachunguza kisa ambapo sokwe anadaiwa kumeza Sh1.9 milioni, katika mbuga moja eneo la Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.

Mashirika ya habari nchini humo yaliripoti kuwa sokwe huyo alivunja na kuingia katika afisi moja, kisha akazila pesa hizo.

Msemaji wa polisi eneo la Kano Abdullahi Haruna alisema kuwa uchunguzi unaendelezwa kubaini ukweli wa madai ya maafisa wa mbuga hiyo.

“Ni kweli kuwa pesa hizo zilipotea katika mbuga ya Kano Zoological Gardens. Pesa hizo zilikuwa za hafla ya siku tano. Tumewakamata wafanyakazi kumi wa mbuga hiyo, ambao wanahojiwa,” akasema Haruna.

Mnamo Februari 2018, mfanyakazi wa bodi moja ya serikali nchini humo alidai kuwa nyoka wa kiroho alitoroka na Sh10 milioni. Mfanyakazi huyo alisema kuwa “Pia mimi nilishtuka. Nimekuwa nikihifadhi pesa katika benki lakini nikaamua kuwa nikiziweka afisini.”

Alisema kila alipofika afisini alipoziweka, hakupata kitu. Alisema baada ya kutafuta kote na kuulizia kutoka kwa watu ndipo aligundua kuwa ‘nyoka wa kiroho’ aliingia na akazimeza.