Michezo

Maafisa wa polisi Afrika Mashariki watua Nairobi kwa michezo

August 25th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAFALME wa voliboli ya wanaume nchini Kenya, GSU, wametaja kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya katika michezo ya Polisi ya Muungano wa Afrika Mashariki (EAPCCO) itakayong’oa nanga jijini Nairobi mnamo Agosti 26, 2019.

Kocha Mkuu Gideon Tarus ametaja Brian Melly kuwa nahodha. Mabingwa mara 13 wa Kenya, GSU, wataanza kampeni yao dhidi ya Tanzania hapo Agosti 28 kabla ya kubana koo na Burundi (Agosti 29) na Uganda (Agosti 30) katika mechi za voliboli ya wanaume ambayo itatumia mfumo wa mzunguko.

Vijana wa Tarus walitwaa taji la mwaka 2018 baada ya kuchapa Tanzania na Burundi nchini Tanzania. Makala ya mwaka huu ni ya tatu. Uganda ilikuwa mwenyeji wa makala ya kwanza mwaka 2017.

Shirika la EAPCCO lilianzishwa mwaka 1998 likijumuisha mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi, Sudan, Sudan Kusini, Rwanda, Djibouti, Eritrea, Ushelisheli, Somalia, Comoros na Ethiopia.

Timu za Tanzania, Rwanda, Sudan na Burundi tayari zimeshawasili kwa mashindano haya yatakayotamatika Septemba 2. Mataifa zaidi yanatarajiwa kufika Nairobi kabla ya mashindano kuanza Jumatatu.

Katika mahojiano ya awali kuhusu uwezo wa GSU kutetea taji la voliboli, Tarus alisema, “Tunajitahidi vilivyo kuhakikisha taji hili linasalia Kenya.”

Naye kocha wa zamani wa GSU, Moses Epoloto, ambaye sasa ni mkurugenzi wa michezo, alikuwa mwingi wa matumaini wanavoliboli wa Kenya watatamba. “Tuna timu nzuri kwa hivyo matumaini ya kuhifadhi taji ni makubwa,” alisema.

Mbali na voliboli, fani zingine katika mashindano haya ni riadha, magongo, ndondi, ulengaji-shabaha, vishale, soka, uogeleaji, handboli, karate, judo na taekwondo.

Kikosi cha voliboli cha GSU (Kenya):

1. David Kirwa

2. Brian Melly (nahodha)

3. Cornelius Rotich

4. Simeon Kipkorir

5. Jacob Kirwa

6. Emmanuel Kogo

7. Cornelius Kiplagat

8. Aboud Chirchir

9. William Kamau

10. Bonfentry Wekesa

11. Andrew Wafula

12. Naftali Chumba

13. Noah Bett

14. Nicholas Matui