Kimataifa

Maafisa wa polisi mashakani kwa kugeuza gari la serikali gesti

February 14th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

SUSSEX, UINGEREZA

MAAFISA wawili wa polisi; wa kiume na wa kike wako kwenye hatari ya kupigwa kalamu, baada ya kutuhumiwa kuwa walifanya ngono katika gari la serikali walipokuwa kazini.

Afisa huyo wa kiume ambaye ana mke na watoto wanne, Inspekta Mkuu Rob Leet, wa miaka 44 anadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu miaka miwili na Sajenti Sarah Porter, 38, ambaye pia wakati wa kisa hicho alikuwa na mume.

Maafisa hao wanadaiwa kuwa waliegesha gari kando ya barabara na wakafanya ngono walipokuwa kazini.

Aidha, walituhumiwa kuwa walikuwa wakisingizia kuwa na kazi kwenye kituo ili wakutane na kushiriki ngono katika vituo vya polisi.

Tume ya kuwachunguza ilifahamishwa kuwa wakati fulani walipokuwa kwenye kawaida yao ya mahaba, Sajenti Porter alikosekana kwa simu, wakati alifaa kuwa katika eneo kulikokuwa na ajali mbaya ya magari.

Wote wanakumbana na mashtaka ya ukosefu wa maadili kazini, ambayo yakidhibitishwa kuwa kweli wote watapoteza kazi baada ya kuhudumu kwa miaka 35, jumla.

Matukio haya yanadaiwa kutendeka kati ya 2014 na 2016. Sakata ya uhusiano baina yao, hata hivyo, ilitoboka Machi 2017 wakati maafisa wenzao wa polisi walianza kushuku kuwa walikuwa wakionana kisiri.

Wadokezi walisema kuwa ijapokuwa wawili hao hawakuwa wakifanya kazi pamoja, mara nyingi walijipanga hivi kwamba uwezekano wa kupatana kila siku ulikuwa juu.

Ilidaiwa kuwa wawili hao wangekutana barabarani na kufanya ngono kabla ya kuendelea na kazi.

“Wangepanga siku zao kwa umakini sana kuunda mkutano usiotarajiwa wakati walipokuwa kazini. Wangekutana maeneo fulani na kufanya ngono ndani ya gari la polisi, mbali na kupatana katika vituo kadha vya polisi,” akasema afisa mnamo 2017.

Bw Leet, hata hivyo, wakati huo alipinga madai hayo, na kusema kuwa ana mke waliyeishi pamoja kwa miaka 22.

Alitumwa kwenye likizo ya lazima tangu madai hayo yalipoibuka, japo Bi Porter aliruhusiwa kurejea kazini.