Maafisa wa polisi wako katika mazingira duni, yaboreshwe – Dkt Mutua

Maafisa wa polisi wako katika mazingira duni, yaboreshwe – Dkt Mutua

Na SAMMY WAWERU

UMEWADIA wakati maslahi ya maafisa wetu wa polisi yaangaziwe na kuimarishwa, amesisitiza gavana wa Machakos, Alfred Mutua.

Dkt Mutua amesema mazingira duni wanayoishi maafisa wa polisi nchini ni mojawapo ya visababishi vikuu vya mmomonyoko wa maadili, miongoni mwao.

Kutokana na majukumu mazito yanayowafika katika kuimarisha usalama, gavana amesema haja ipo watunzwe vyema na kuhakikisha shida zao zinatatuliwa.

“Ni muhimu tuambiane ukweli, mazingira ya kazi na wanayoishi maafisa wetu wa polisi ni duni,” Dkt Mutua akasema.

“Nyumba wanazoishi ni duni, zimechakaa ilhali wana familia. Maeneo yao ya kazi ni mabovu. Kimsingi, Kenya maslahi ya maafisa wa usalama yamepuuzwa,” akaelezea.

Akilinganisha mazingira ya humu nchini na ya Marekani, gavana Mutua anasema kuna tofauti kubwa, gapu anayohoji isipoangaziwa uhusiano wao na umma utazidi kuwa mbaya.

“Nimeishi Marekani, maslahi ya maafisa humo yameangaliwa vyema kabisa. Mbali na kuwepo kwa mazingira bora ya kazi na kuishi, bima ya afya miongoni mwao imepewa kipaumbele,” akasema.

Dkt Mutua na ambaye anahudumu awamu yake ya pili Machakos, alisema alipochukua hatamu ya ugavana, miongoni mwa sera zake ilikuwa kuboresha mazingira ya utendakazi wa polisi.

“Tumewajengea nyumba bora za kuishi. Ni wenzetu, tunapopata shida huwakimbilia,” akadokeza.

Dkt Mutua alitoa kauli hiyo kutokana na kisa cha hivi majuzi cha afisa wa polisi, Caroline Kangogo, ambaye amegonga vichwa vya vyombo vya habari kwa kuua kinyama wanaume wawili.

You can share this post!

Wakazi wa Lamu walia makali ya njaa, kiu

Namna rahisi ya kuandaa Pizza