Habari Mseto

Maafisa wa utawala wa kimaeneo kuwasaka na kuwapeleka wanafunzi kidato cha kwanza kwa lazima

January 24th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

SERIKALI inalenga kuwatumia machifu na wanachama wa Nyumba Kumi kuwatafuta wanafunzi ambao walifanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka 2019 lakini hawajajiunga na shule za upili.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema kuwa wakati wa shughuli hiyo, wanafunzi hao watapelekwa katika shule za upili zilizo karibu kwa nguvu, ili kufanikisha mpango wa serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanaomaliza shule ya msingi wanajiunga na shule za upili.

Hapo jana, waziri alithibitisha kuwa sio wanafunzi wote 1,075,201 waliofanya KCPE wamejiunga na Kidato cha Kwanza, licha ya wizara kuongezwa muda wa kuripoti kwa wiki moja.

Mpango huo ulizinduliwa mwaka uliopita na Rais Uhuru Kenyatta, kama mojawapo ya mikakati kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi anayekosa kusoma kwa kisingizio cha kukosa karo.

Akizugumza katika shule ya upili ya wasichana ya State House Girls Nairobi alipoizuru Prof Magoha alisema ni wanafunzui 850,000 waliokuwa wamejiunga na kidato cha kwanza.

Lakini kufikia Ijumaa jioni idadi ya wanafunzi watakaokuwa wamejiunga na kidato cha kwanza kote nchini itafikia 920,000.

“Kungali na wanafunzi kati ya 150,000 na 200,000 ambao watasakwa kutoka nyumbani kwao. Mwongozo wa Serikali kwamba wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane ni mwafaka kabisa na umefaulu,” alisema waziri huyo.

Wakati wa shughuli hiyo itakayofanyika kote nchini, maafisa wa utawala kimaeneo wameagizwa wawapeleke wanafunzi watakaonaswa katika msako huo kwa shule za upili zilizoko karibu nao.

Lakini alisema wanafunzi ambao wameamua kwa hiari kurudia darasa la nane wako huru kufanya hivyo.

Mafunzo ya kiufundi

Pia alisema wanafunzi wenye umri mkubwa watakaoamua kujiunga na vyuo vya Mafunzo ya Kiufundi (Tvet) wataruhusiwa kwenda na hawatashurutishwa kujiunga na kidato cha kwanza.

“Kuna wazazi na wanafunzi ambao wameamua watarudia darasa la nane. Uamuzi huo hatuupingi lakini idadi ya watakaorudia darasa la nane itasemwa.Kuna wanafunzi waliokomaa na wameamua kujiunga na vyuo vya ufundi. Wako huru kujiunga na Tvet’s,” alisema Prof Magoha.

Kuhusu wasichana waliofunga ndoa badala ya kujiunga na kidato cha kwanza, Waziri alisema maafisa wa utawala wa mikoa wameagizwa watamatishe ndoa hizo na wasichana hao kupelekwa shule za upili zilizo karibu kwa lazima.

Maafisa wa utawala watawapeleka baadhi ya kwa shule za mabweni ndipo wapate ulinzi unaofaa’

“Wasichana wajawazito watajiunga na shule na wakati wa kujifungua ukiwadia watapewa fursa ya kupumzika kisha warudi shuleni kuendelea na masomo,” alisema waziri Magoha.

Waziri aliwataka walimu na wakuu wa shule waimarishe shule zao kuhakikisha wanafunzi wote wametoshea.

Aliwatadharisha wakuu wa shule za upili dhidi ya kuwafukuza wanafunzi akisema jambo hilo ni kitendo cha uhalifu na mmoja atachukuliwa hatua za kisheria