Habari

Maafisa waadilifu wa trafiki kutuzwa

July 9th, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

[email protected]

INSPEKTA Jenerali wa Polisi, Hillary Mutyambai ameahidi kuanzisha mpango wa kuwatuza maafisa wa trafiki watakaotekeleza wajibu wao bila kujiingiza katika visa vya ufisadi.

Akiongea Jumanne akiwa katika eneo la Murakha katika barabara yenye shughuli nyingi ya Kakamega-Kisumu, IG, amesema analenga kuhakikisha maafisa wa trafiki hawapokei au kuitisha hongo kutoka kwa wenye magari.

“Nimewazia kuwatuza trafiki watakaotoa mfano wa kuigwa kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuhakikisha kuhakikisha barabara zetu ni salama,” amesema Mutyambai ambaye yuko kwenye ziara katika Kaunti ya Kakamega.

Amemsifu Kamanda wa Polisi wa eneo, Bw Bernard King’oo pamoja na maafisa chini yake kwa kufanya kazi ya kuridhisha.

“Nataka maafisa wa trafiki hapa Kakamega kuwa mfano kwa wengine na hata napanga kuwaalika kutagusana na walio katika maeneo mengine na kuwaeleza ni jinsi gani wanaweza kuwa mfano wa kuigwa,” amesema Mutyambai.

Wenye magari na pikipiki waliokiuka sheria na kanuni za trafiki wamekamatwa eneo la Murakha na kushtakiwa katika mahakama tamba iliowekwa kando ya barabara hiyo ya Kakamega-Kisumu.

Baadaye Mutyambai pia amekutana na makamanda wa polisi kutoka eneo la Magharibi kwenye kikao cha faragha na baadaye akamtembelea Kamishna wa eneo Bi Anne Ngetich na Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.

IG anatarajiwa kufungua Sacco ya maafisa wa polisi, tawi la Kakamega kabla ya kuelekea Matungu ambako kumekuwa na operesheni ya kurejesha hali ya usalama kwa muda ambao unaingia mwezi wa pili sasa.