Habari za Kaunti

Maafisa wachunguza vifo vya watu wawili Makadara

March 28th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO katika Kaunti ndogo ya Makadara wanachunguza visa viwili kuhusu watu wawili kufariki katika maeneo tofauti.

Naibu Kamishna wa Makadara Philip Koima aliambia Taifa Leo kuwa mtu mmoja alikufa maji alipokuwa akielekea nyumbani.

Kulingana na afisa huyo, mwendazake alikumbana na kifo alipojaribu kuvuka sehemu ya barabara ya Sosio iliyofurika maji eneo la Corner katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Donholm, eneo la Industrial Area.

Katika kisa cha pili, kamanda wa polisi Makadara Bi Judiith Nyongesa, alisema wapelelezi wanachunguza kisa ambapo mwanamume mmoja alikumbana na kifo katika eneo la ujenzi lililoko eneo la Sanasana ndani ya mtaa wa Plainsview, tarafa ya South B katika Kaunti ndogo ya Starehe.

Inadaiwa Bw Godfrey Savata,29, alinaswa na umeme alipokuwa kazini katika orofa ya nne ya jumba linaloendelea kujengwa.

Alianguka chini kwa bahati mbaya na kufa kutokana na majeraha.

Bi Nyongesa aliongeza kwamba mwili wa marehemu ulikuwa na jeraha kichwani na mkono ulikuwa umeteketea.

Polisi waliupeleka mwili huo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City.

“Tulichopokea kutoka kwa Bw Harrison Muasya, msimamizi katika jumba linalojengwa Saika kupitia Chumba cha Mawasiliano ya polisi Nairobi, ni kwamba mtu fulani alikuwa ameanguka kutoka kwa orofa ya nne ya jengo ambalo ujenzi wake ulikuwa ukiendelea,” Bi Nyongesa akasema.