Habari za Kitaifa

Maafisa wafanikiwa kufurusha majangili na kurejesha utulivu Baringo


20HALI ya utulivu imerejea katika maeneo yaliyohangaishwa na majangili Kaunti ya Baringo huku timu ya vikosi vya usalama inayoendesha oparesheni kali eneo hilo ikionekana kufanikiwa kuwafurusha wahalifu.

Haya yamejiri baada ya vikosi vya usalama kulipua milima hatari ya Korkoron, mabonde ya Tandare na Ng’elech, kuimarisha uangalizi angani na doria kwenye maficho ya majangili.

Eneo hilo lenye wingi wa malisho kwa mifugo lilikuwa limegeuzwa bustani ya majangili waliovamia na kuwafurusha makwao wakazi na kusababisha vijiji kadhaa kuachwa mahame.

Tangu 2021, wahalifu waliojihami wamevamia maeneo hayo ya Baringo Kusini, wakipora maelfu ya mifugo wakijifanya kusaka maji na malisho kabla ya kutekeleza mashambulizi ya kikatili na kuwafurusha wakazi makwao.

Vilima vya Korkoron vipo mkabala na vijiji kadhaa ikiwemo Kasiela huku upande mwingine ukiwa Bonde la Ng’elecha lililogeuzwa pango la majangili ambapo mifugo wa kuibwa hufichwa kwa sababu hakuna anayeweza kujaribu kufika huko.

Majambazi wanaojificha kwenye vilima na mabonde wamesababisha vifo vya idadi isiyojulikana ya watu na kuwafurusha maelfu katika vijiji vya Kitorongon, Menmeno, Seretion, Chepng’anian, Kapsikwon, Lomulel, Korkoron, Kapkechir, Tuiyotich, Korkoron, Lamaiywe, Karne, Tuiyotich, Kapkechir, Tandar, Sinoni, Kasiela, Arabal na Kapindasum.

Maeneo hayo yanayosheheni majambazi hayana barabara huku mazingira yake mabovu yakiwarahisishia kazi wahalifu wanaoketi kwenye vilele vya vilima kutazama na kuzunguka wahasiriwa.

Sehemu hizo zimezingirwa na magofu ya vijiji kadhaa ambavyo wenyeji wake walitoroka kutokana na misururu ya mashambulizi.

Licha ya hayo, timu ya vikosi jumuishi imeonekana kufanikiwa kuwafurusha majambazi hao waliojihami na kurejesha usalama maeneo hayo hatua ambayo imewezesha wenyeji waliofurushwa kumiminika wakirejea makwao.

Machi 2023, vikosi vya usalama vinavyoendesha oparesheni kaunti hiyo vililipua vilima vinavyohofiwa vya Korkoron na Tandare katika juhudi za kuwafurusha majangili katika maeneo yaliyoorodheshwa na serikali kuwa maficho ya majambazi.

Serikali iliwaagiza raia wanaoishi Tandare, Korkoron, Karau, Vilima vya Ng’elecha, Ramacha, mapango ya Rugus, Losokoni, Miamba ya Laramoru na Amaya Gorges na Bonde la Noosidan, kuhama.

Kulingana na Kamanda wa Polisi Kaunti ya Baringo, Julius Kiragu, kambi ya maafisa wa polisi wa Kitengo cha (GSU) iliyoanzishwa mwaka jana kwenye shina la vilima vya Korkoron katika kijiji hatari cha Lamaiywe ilichangia pakubwa kuwafurusha washambulizi hao waliojihami.

“Serikali ilituma vikosi viwili vya maafisa wa GSU kijijino Lamaiywe ili kurejesha utulivu na kuwezesha watu kurejea makwao. Kwa usaidizi wa vikosi mbalimbali vinavyotekeleaza oparesheni ya usalama eneo hilo, tuliendesha pia uangalizi angani uliotuwezesha kufuatilia maeneo ambapo majangili hao walijificha,” Bw Kiragu alieleza Taifa Leo.

“Tunapozunguza, maeneo hayo sasa ni salama na wenyeji waliokuwa wamefurushwa wamerejea makwao.”

Maafisa 70 wa Polisi wa Akiba (NPR) wametwikwa jukumu la kushika doria katika vijiji zaidi ya sita vilivyosalia mahame na vinavyoshukiwa kuwa maficho ya majangili ambapo huzunguka mwendo wa zaidi ya kilomita 30 kwa mguu kila siku.