Habari Mseto

Maafisa wafanya msako mkali dhidi ya pombe haramu waking’oa milango

January 19th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

VITA dhidi ya pombe haramu viliendelea Alhamisi ambapo msako mkali uliendeshwa na maafisa wa utawala katika eneo la Budalangi lililoko kwenye mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba katika tarafa ya South B, Kaunti ya Nairobi.

Akiongea na Taifa Leo, naibu kamishna wa Starehe John Kisang alithibitisha operesheni hiyo iliongozwa na machifu na manaibu wao chini ya kinara wa tarafa ya South B Solomon Muraguri na mwenzake Bw Samuel Kimeu Ndambuki mapema asubuhi.

Bw Kisang alisema maafisa wake walifanikiwa kuvamia na kupata nyumba 10 zilizotumiwa kama ‘baa’ za kuuzia vileo haramu.

Aliongeza kwamba washukiwa tisa walikamatwa wakati wa operesheni hiyo iliyoshirikisha pia viongozi wa mitaa na kamati za Nyumba Kumi.

“Kikosi changu kilifanikiwa kupata nyumba 10 zilizokuwa zikitumiwa kuuzia watu pombe haramu na pia ni ‘baa’ ambazo hazina leseni. Walinasa lita 320 za pombe aina ya mugasha na pia lita 70 za chang’aa ambayo iliharibiwa,” Bw Kisang akasema.

Vilevile, waliharibu vifaa vyote vilivyotumiwa katika mchakato mzima katika biashara hiyo iliyopigwa marufuku kote nchini na serikali.

Maafisa wa utawala wakiendeleza operesheni dhidi ya pombe haramu katika eneo la Budalangi lililoko kwenye mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba katika tarafa ya South B, Kaunti ya Nairobi. PICHA | SAMMY KIMATU

Kadhalika, machifu waling’oa milango yote katika kila nyumba ambazo zilikuwa zinatumika kama stoo za kuwekea pombe haramu.

Waliichukua pombe hiyo na kuibeba.

“Mbinu ya kung’oa milango hutusaidia pakubwa kupambana na wauzaji wa chang’aa. Kwanza mmiliki wa nyumba atazozana na mpangaji kuhusu milango ya nyumba kupotea. Baadaye, mpangaji atalazimika kuwajibika na hatimaye suluhu ya mzozo wao ni ahame akapange nyumba kwingineko. Akianza tena kuuza pombe atakakohamia, atajutia makosa yake kwani huko pia atapambana na maafisa wa serikali kwenye maeneo hayo,” akaeleza.

Aliongeza kwamba misako iaidi itaendelea wakilenga kuwanasua vijana wengi waliozama katika ulevi kupindukia badala ya kujihusisha katika ujenzi wa taifa.

Alishauri vijana kuungana katika makundi yaliyosajiliwa ndiposa wapate mikopo kujiendeleza kupata mapato.