Maafisa wahofia wagonjwa huiba vyandarua vya mbu

Maafisa wahofia wagonjwa huiba vyandarua vya mbu

Na SHABAN MAKOKHA

MAAFISA wa Afya katika hospitali moja ya eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega, wameelezea hofu yao kuwa wagonjwa wanaolazwa kwenye wodi huiba vyandarua hali inayowaweka wagonjwa wengine katika hatari ya kuambukizwa malaria.

Haya yalijiri baada ya msimamizi mmoja wa hospitali hiyo, Bi Mwanaisha Awinja , kulalamika kuwa ana mgonjwa mjamzito ambaye anatarajiwa kutumia chandarua kutokana na hali yake.Wagonjwa waliopatikana na malaria walihofia jinsi watakavyojikinga dhidi ya ugonjwa huo ikiwa kuna uhaba wa vyandarua katika hospitali hiyo.

Wengi waliolazwa hospitalini walipatikana na malaria. Mmoja wao akiwa Bi Jennifer Nafula, 24, ambaye alilalamika kuwa wengi walipatikana na ugonjwa huo kutokana na ukosefu wa vyandarua.“Mimi pamoja na wagonjwa wengine tulilazwa hospitalini kutokana na malaria kwa kuwa hatuna vyandarua nyumbani.

Tunashangaa tutajikingaje dhidi ya malaria ikiwa hospitali haina vyandarua,” Bi Jennifer aliambia Taifa Leo.Wagonjwa hao walitoa malalamishi yao wakati Mbunge wa Matungu, Bw Peter Nabulindo, alipotembelea kituo hicho ili kukagua hali ya utoaji huduma hasa baada ya hospitali hiyo kuangaziwa kwa kutotoa huduma bora za kiafya kwa wagonjwa.

Msimamizi wa hospitali hiyo, Bw Hillary Keverenge, alisema kuwa wagonjwa waliolazwa huiba vyandarua hivyo pindi tu wanapoachiliwa kurudi nyumbani baada ya kupata nafuu.“Wagonjwa waliolazwa kwenye wodi hutoka na vyandarua hivyo baada ya kupata nafuu.

Nyengo zinazoshikilia vyandarua hivyo ziko bure,” alisema Bw Keverenge akimwonyesha mbunge huyo alipotembelea kituo hicho.Bw Keverenge alisema kuwa waliwekeza pesa nyingi kununua vyandarua hivyo na ikafika wakati ambapo bajeti yao haingewaruhusu kununua vyandarua tena.

Msimamizi huyo alisema kuwa wananchi wanahitaji kuhamasishwa kuhusu athari za kuviiba vyandarua hivyo katika utoaji huduma wa hospitali.Mbunge huyo aliitaka Wizara ya Afya kugawa vyandarua kwa wamama wajawazito na wanaojifungua katika vituo mbalimbali vya afya.

Bw Nabulindo aliahidi kutafuta msaada kutoka kwa mashirika husika na idara za serikali katika kutafuta vyandarua na kuzisambaza kwa kaya zinazostahili katika eneo bunde hilo.

  • Tags

You can share this post!

Wakili wa Ruto kuapishwa wiki ijayo kumrithi Bensouda

Miradi ya Uhuru Nyanza inavyotishia kuchimbia Raila kaburi...