Habari za Kitaifa

Maafisa wakuu wa serikali kuzimwa kutumia Tiktok – Kindiki

March 21st, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI haitapiga marufuku matumizi ya mtandao wa kijamii wa TikTok lakini itawazima maafisa wake wakuu ili wasitumie jukwaa hilo kusambaza habari muhimu za serikali.

Hii ni kutokana na sababu za kiusalama.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki mnamo Alhamisi aliwaambia wabunge kuwa matumizi ya mtandao huo nchini yamekuwa hatari kwa usalama wa nchi kwa sababu hauzingatii Sheria ya Kulinda Data.

Hata hivyo, alitambua umuhimu wake haswa kwa watumiaji wa TikTok kwa shughuli za kuwaletea mapato kama vile wasanii wa fani mbalimbali.

“Licha ya kuwepo kwa hatari hii, serikali haitachukua hatua ya haraka ya kupiga marufuku matumizi ya Tiktok. Itahakikisha kuwa imezingatia Sheria ya Kulinda Data na Kanuni husika. Sababu ina umuhimu wake katika jamii ya sasa. Lakini maafisa wakuu wa serikali hawataruhusiwa kutumia mtandao huo kupitishia habari za serikali,” Prof Kindiki akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Kusikiza Maombi kutoka kwa Umma.

Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai.

“Suala kuhusu nani anapasa kuutumia na namna ambayo mtandao huo unapasa kutumiwa nchini ni mojawapa ya mada ambazo hujadiliwa katika Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC). Hii ni kwa sababu wizara yetu ndio hushirikisha mipango ya kudhibiti uhalifu mitandaoni,” Profesa Kindiki akaongeza.

Waziri alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kuhusiana na ombi Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya kutoa ushauri ya Bridget Connect Consultancy Bob Ndolo kwamba wabunge wapendekeze kupigwa marufuku kwa TikTok nchini.

Bw Ndolo alisema kuwa mtandao huo unavuruga tabia za vijana kuwawezesha kufikia taarifa, video na picha chafu.

“Ingawa matumizi ya Tik Tok ni maarufu haswa miongoni mwa vijana nchini, yale maudhui yanayosambazwa si mazuri kwani yanasheheni vita, jumbe zisizo za staha, video na picha za ngono. Maudhui ya aina hiyo huvuruga maadili ya vijana. Hali hii ni tishio kwa mila na tamaduni za jamii mbalimbali za humu nchini,” Bw Ndolo akasema kwenye ombi lake lilisomwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula mnamo Novemba 2, 2023.

Siku moja baada ya kuwasilishwa ombi hilo, Rais William Ruto alisema mambo hasiyofaa na yanavuruga maadili yataondolewa katika jukwa la TikTok, huku akitetea matumizi yake.

Alisema hayo baada ya kufanya mazungumzo na afisa mkuu mtendaji wa kampuni inayomiliki mtandao huo wa kijamii Shou Zi Chew.

Wakati wa mkutano huo, uliofanywa kwa njia ya mtandao, Rais Ruto alisema kuwa serikali itashirikiana na TikTok katika mpango wa kuhakikisha kuwa mambo yasiyofaa yanaondolewa katika jukwaa lake.

“Afisa Mkuu Mtendaji wa TikTok Zi Chew amenihakikishia kuwa wataondoa maudhui yale yote mabaya na kuzingatia sheria zote zinakinga watumiaji wa mtandao dhidi ya kuingia katika hatari,” kiongozi wa taifa akaeleza.