Habari Mseto

Maafisa waliolinda mlingoti wa Safaricom wajeruhiwa na magaidi Turkana

October 3rd, 2020 2 min read

Na SAMMY LUTTA

MAAFISA wawili wa polisi wa kitengo cha RDU waliokuwa wakilinda mlingoti wa kampuni ya Safaricom katika kijiji cha Lomelo, Turkana Mashariki walijeruhiwa vibaya na magaidi waliowashambulia mnamo Jumamosi.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Turkana, David Mburukuwa, amesema kwamba afisa mmoja wa polisi alipigwa risasi na magaidi hao kwenye miguu yote miwili huku mmoja akipata majeraha mabaya ya risasi kwenye sehemu ya kushoto ya shingo.

Shambulio hilo lilifanyika mapema saa tatu asubuhi.

“Maafisa wa RDU katika eneo la Lomelo waliwasili haraka katika eneo la tukio na kuwaokoa wenzao,” akasema Mburukuwa.

Alisisitiza kwamba usalama umeimarishwa zaidi katika eneo hilo baada ya maafisa wa zaidi kutoka kitengo cha polisi wa kawaida, GSU na polisi wa akiba wamepelekwa katika kijiji cha Lomelo ili kukabiliana na makundi ya majambazi na magaidi ili kukomesha visa vya utovu wa usalama.

Julius Ereng, ambaye ni miongoni mwa wafanyakazi katika eneo linakosimikwa mlingoti huo wa Safaricom, alisema wavamizi hao wa kigaidi awali walikuwa wakilenga maafisa wa polisi.

Kwa mujibu wa Ereng, wao waliamka vizuri kwa minajili ya kuendeleza shughuli zao za kazi kabla ya milio ya risasi kuanza kusikika hewani majira ya saa tatu.

“Tulilala ardhini maafisa walipoanza kukabiliana na majambazi hao kabla ya maafisa zaidi wa usalama kufika katika eneo la tukio na kuwapiga jeki wenzao. Nusura afisa mmoja wa polisi auawe baada ya risasi iliyofyatuliwa kumpata begani,” akasema Ereng.

Kwa upande wake, Caxton Edome ambaye ni mkazi wa eneo la Lomelo, alisema mlingoti wa Safaricom ulipania kuimarisha huduma za mawasiliano na uvamizi huo ni njia ya magaidi kulalamikia ujenzi wa mtambao huo.

“Tunahitaji sana mlingoti huu ambao utatumiwa na Safaricom kutuletea huduma za mawasiliano ili tupate jukwaa la kutoa habari za mara kwa mara kuhusu usalama wetu kwa mamlaka husika,” akasema Edome kwa kutaka serikali kuimarisha zaidi usalama kwa kuajiri maafisa zaidi wa polisi na kuwatuma katika eneo hilo.

Shambulio hilo lilisitisha huduma za usafiri kwa muda katika Barabara ya Kapedo na Lomelo.

IMETAFSIRIWA NA: CHRIS ADUNGO