Makala

Maafisa walipuuza dokezi muhimu za kumkamata mshukiwa wa mauaji ya Jayne Murage?

July 20th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

JANUARI 26, 2017, Bi Jayne Nduta Murage akiwa na umri wa miaka 40 na mama wa watoto watatu aliondoka kazini alikokuwa mhudumu wa baa mwendo wa saa nne na nusu usiku.

Aliyehitimu elimu ya darasa la nane mwaka wa 1992 kutoka shule ya msingi ya Watuha iliyoko katika Kaunti ndogo ya Kangema ndani ya Kaunti ya Murang’a, alikuwa akifanya kazi katika baa ya Joyland iliyoko katika mji wa Kaharati katika kaunti hiyo.

Alikuwa ametoroka kutoka ndoa yake ya miaka 10 mwaka wa 2012 na ambapo alikuwa mke halali wa Bw Patrick Maina ambaye walikuwa wamevishana pingu za maisha katika kanisa Katoliki la Kiangunyi mwaka wa 2002.

Kama ilivyokuwa kawaida yake, baada ya kutoka kazini, alikuwa ama akiabiri magari ya uchukuzi wa umma, kuomba lifti au kutumia usafiri wa bodaboda kufika nyumbani kwake alikokuwa amepanga katika mji wa Maragua ulioko takribani kilomita 10 kutoka Kaharati.

Siku ya tukio, hakufika nyumbani kwake na badala yake, watoto waliokuwa wakienda shule asubuhi iliyofuata ndio walimpata akiwa ametupwa kichakani, mwili wake ukiwa uchi, akiwa hafifu na aliyekuwa amelemewa na majeraha.

Kilichofuata ni uchunguzi – unaotajwa kuwa duni – wa maafisa wa polisi ambao waliishia kumnyima Bi Murage haki ikizingatiwa kuwa aliaga dunia wiki moja baadaye.

Hii ni licha ya kuwa kulikuwa na dokezi chungu nzima za kusaidia maafisa wa uchunguzi kufuatilia kesi hii na kunasa mshukiwa au washukiwa.

Taifa Leo iliripoti mauti hayo na kisha kufuatilia mazishi yake na sasa imeendelea kuwa chonjo kusaka dokezi.

Kwa mujibu wa aliyekuwa kamanda wa Polisi wa Murang’a Bi Naomi Ichami, Bi Murage alikuwa amenyongwa kwa koo, akagongwa na kifaa butu kichwani na kubakwa pia.

Baya zaidi ni kwamba aliyemtekelezea unyama huo alimwingiza kipande cha mti, ashakum si matusi, kipande cha mti katika sehemu za siri na kukiacha hapo.

“Alikuwa katika hali mbaya wakati maafisa wa kituo cha polisi cha Maragua walimleta katika hospitali hii ya Maragua. Alikuwa na uhai ndio, lakini hali ya dharura,” anasema Bw James Mwangi, muuguzi katika hospitali hiyo ya Maragua.

Anasema kuwa Bi Murage hakupata huduma ya daktari kwa kuwa “madaktari walikuwa wakishiriki mgomo wao wa kitaifa.”

Anasema kuwa Bi Murage alikaa katika hospitali hiyo kwa siku nne na baada ya kupoteza uwezo wa kuongea, jamaa wake wakamtoa ili wakasake matibabu katika hospitali za kibinafsi.

Ndipo alipelekwa katika hospitali za Kiriaini, Kimkan na Outspan bila ufanisi wowote na ambapo aliishia kuaga dunia baada ya wiki moja.

Baadhi ya vijana wanaohudumu katika sekta ya bodaboda wakishirikisha utazamaji wa mwili wa Bi Jane Murage katika mochari ya Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Alizikwa Februari 14, 2017, katika shamba la mumewe.

Kwa mujibu wa aliyekuwa kamanda wa kitengo cha uchunguzi wa Jinai Kaunti ya Murang’a, Julius Rutere, kifo cha Bi Murage kilikumbwa na dosari ya ukosefu wa mashahidi wa kutoa habari za kuwezesha kunaswa kwa washukiwa.

Hata hivyo, Bw Mwangi anasisitiza kuwa “hakukuwa na nia ya kujituma kutekeleza uchunguzi.”

Anasema kuwa hakuna uchunguzi ambao maafisa hao walitekeleza kuonyesha kuwa walikuwa na nia ya kutafuta haki.

“Hawakupiga mwili huo picha, hawakuchukua alama za vidole kutoka kwa mwili huo na hata hawakuleta nguo zake ambazo zilikuwa kando ya mwili wake katika eneo la uvamizi,” anasema.

Aidha, anasema kuwa jamaa wa mwathiriwa waliruhusiwa kumuosha hivyo basi kuondoa ushahidi muhimu kutoka kwa mwili wake hasa katika sehemu ya siri.

Aidha, maafisa hao hawakuweka vikwazo vya kutembelewa kwa mwathiriwa huyo akiwa hospitalini kwa minajili ya kumkinga kutokana na uwezekano wa aliyekuwa amemvamia kuingia hapo na “kummaliza baada ya kugundua hakuwa ameaga dunia.”

Kuhifadhi ushahidi

Anasema kuwa hata hakuna afisa aliyeagiza hospitali hiyo kuhifadhi ushahidi wowote kutoka kwa mwili wa mwathiriwa “kumaanisha walikuwa wakichukulia kisa  hicho kwa ulegevu wa kimawazo ndani ya utendakazi wao.”

Bi Ichami anasema kuwa “ni ukweli kisa hiki kilikumbwa na changamoto tele za uchunguzi.”

Kwa mfano, anasema kuwa uchunguzi ulizinduliwa wiki moja baadaye baada ya Bi Murage kuaga dunia.

“Ndani ya wiki hiyo moja, kulikuwa kumenyesha hivyo basi kuharibu ushahidi katika eneo la uvamizi na pia watu walikuwa wamekanyaga eneo hilo wakilitembelea kujionea alikopatikana Bi Murage,” anasema.

Anasema shida kubwa ni kuwa, uchunguzi ulianza Bi Murage akiwa ameaga dunia tayari na ambapo hakuwa ameandikisha taarifa yoyote ya kutoa dokezi ya nani alimvamia.

Anakiri kuwa washukiwa wanne waliishia kukamatwa ndio, lakini hakuna yeyote aliishia kuhusishwa na ushahidi kama aliyemvamia Bi Murage.

Anasema kuwa uchunguzi ulionyesha kuwa Bi Murage alifika katika baa nyingine inayofahamika kama Mid Way na ambayo iko takribani kilomita tatu kutoka ile baa ya Joyland.

“Alifika hapo akiwa ameabiri gari dogo na ambalo tulinasa dereva walo pamoja na wengine watatu wanaume ambao walionekana ndani ya baa hiyo wakiwa na Bi Murage,” anasema.

Anaongeza kuwa hakuna ushahidi wowote uliwaweka wanne hao ndani ya mtego wa kuwa washukiwa wa kuandamwa.

Lakini sasa, uchunguzi wa Taifa Leo , kulingana na fununu ni kwamba kuna mshukiwa mkuu katika mauaji ambaye alikuwa na uhusiano wa karibu na Bi Murage. Ni mhudumu wa bodaboda.

Mwajiri wa awali wa Bi Murage, akifahamika kama Leah Mwangi anasema kabla ya Bi Murage kuishiwa na uwezo wa kuongea, alikuwa “amenifahamisha kuwa mhudumu huyo wa bodaboda ndiye alikuwa amehusika.”

“Niliambia maafisa wa polisi hivyo lakini walichukua namba yangu ya simu wakisema kuwa wangeniita lakini sijawahi kupata mwito huo,” anasema Leah Mwangi.

Mmoja wa wahudumu katika baa ya Mid Way anatoa maelezo yanayoelekea kuwa sawa na ya Leah Mwangi.

“Tumekatazwa kujiingiza kwa suala hilo,” anasema mhudumu huyo ambaye hataki jina lake lichapishwe.

Na maafisa wa polisi hawajawahi kufika katika baa hiyo kuuliza maswali kuhusu tukio hilo lililoishia mauti kwa Bi Jayne Nduta Murage.