Habari Mseto

Maafisa wanaoiba kahawa viwandani waonywa vikali

October 23rd, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

MAAFISA wa viwanda vya kahawa Kaunti ya Muranga wameonywa dhidi ya kushirikiana na wezi wa kahawa inayohifadhiwa viwandani.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti Muranga, Mohammed Barre, visa vyote vya wizi vimekuwa na matukio sawa ambapo walinzi wanafungwa kwa namna zinazofanana kabla ya wezi kutoweka na zao hilo la wakulima.

Alieleza kwamba sehemu kubwa ya maafisa hao hushirikiana na wezi na kutoa wito kwa wakulima kuwaondoa maafisa wao kupitia uchaguzi kila visa vya wizi vinapotokea viwandani mwao.

Akizungumza wikendi, Bw Barre alishangaa ni vipi wezi hao huweza kuingia viwandani na kwenda moja kwa moja ghalani, kuwafunga walinzi, kupakia gredi bora ya kahawa na kuondoka bila kugunduliwa.

“Mambo haya ni sharti yakome, maafisa fisadi wa viwanda vya kahawa wamo katika darubini yetu na yeyote atakayekamatwa kwa kuwaibia wakulima maskini wasio na hatia atakabiliwa na makali ya sheria,” alionya vikali.

Aidha, alisema kikosi cha ulinzi kilikuwa makini maadamu msimu wa kuvuna kahawa ulikuwa karibu, akisema doria zilizoimarishwa zitashuhudiwa kama mojawapo ya hatua za kudhibiti visa vya wizi wa kahawa ambavyo vimeathiri eneo hilo kwa muda mrefu.

“Tunaelekea msimu wa kuvuna kahawa na maafisa wa viwanda vya kahawa wanapaswa kujihadhari kuhusu wizi wa zao la wakulima. Hatuwezi kuruhusu hali ambapo wakulima wanawekeza mashambani mwao na kisha wafisadi wanauza kahawa yao kwa kisingizio kwamba imeibiwa,” alisema Kamishna.

Alisisitiza vilevile haja ya usimamizi thabiti wa viwanda vya kahawa ili kuwezesha wakulima kupata malipo bora akisema, kahawa ingali na soko kubwa ulimwenguni ikiandamana na malipo bora.

Mwezi uliopita, Serikali ya Kaunti Muranga ilitangaza mipango ya kuunganisha viwanda vyote vya kahawa ili kuendesha shughuli chini ya Muungano wa Mashirika ya Wakulima wa Kahawa Muranga katika juhudi za kufufua sekta hiyo.

Alizungumza katika mkutano na wajumbe kutoka viwanda vyote 146 vya kahawa.