Habari

Maafisa wanne wakamatwa kwa kuvamia makazi ya Midiwo

February 11th, 2020 1 min read

Na JUSTUS OCHIENG

 

MAAFISA wanne wa polisi wamekamatwa baada ya tukio la Jumatatu ambapo walivamia makazi ya mbunge wa zamani wa Gem Jakoyo Midiwo yaliyoko Mtaani Milimani, Kisumu ambapo walimdhalilisha kufuatia tofauti iliyoibuka baina yao na dereva wake.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisumu Ranson Lolmodooni amethibitisha kutiwa mbaroni kwa wanne kufuatoa tukio hilo lililojiri mapema Jumatatu.

“Tumewakamata maafisa wanne waliohusika katika tukio hilo ambapo watatu ni wanaume na mwingine mwanamke na tunaendelea na uchunguzi,,” amesema Bw Lolmodooni leo Jumanne.

Midiwo amesema alipoteza simu katika vuta n’kuvute baina ya maafisa na dereva wake iliyoanzia Kisumu mjini hadi nyumbani kwake.

Naibu huyo wa zamani wa kiranja wa bunge la kitaifa amesema alipoteza simu.

Midiwo ameambia ‘Taifa Leo’ aliamshwa na mlinzi wake wa usiku.

“Nilikuwa nimelala mlinzi wa usiku alipokuja akaniamsha ambapo niliwaona maafisa watano; watatu wanaume na wawili wanawake; na nilipowauliza sababu ya uwepo wao, mmoja alinirukia na akaanza kunikaba,” amesema Midiwo.

Afisa mmoja, ameeleza Midiwo, alimtambua na akajaribu kuingilia kati bila mafanikio.

“Aliniambia walikuwa wamelewa,” ameeleza Midiwo akisema walimlazimisha kuingia kwa gari aina ya Probox na kumzuilia katika seli za kituo cha Central.

Baadaye asubuhi afisa anayesimamia kituo (OCS) na afisa wa kutoa amri katika kitengo cha polisi (OCPD) walifika ambapo walimuachilia.

 

Amesema amepata P3 pamoja na dereva wake Bw Elijah Ochieng’ na wako tayari kukutana na maafisa hao mahakamani mkono wa sheria uchukue hatua yake.

“Nimepigiwa pia na Mamlaka Huru ya Kuwachunguza Maafisa wa Polisi (Ipoa) na nitawapa malalamiko,” amesema Bw Midiwo.

Kamanda wa Polisi eneo la Nyanza Dkt Vincent Makokha amesema washukiwa wamekamatwa na watawasilishwa mahakamani Jumatano.

“Kamanda katika Kaunti anashughulikia suala hili na watafikishwa mahakamani,” amesema Dkt Makokha.