Maafisa wapata ng’ombe kadhaa walioibwa kutoka Nakuru wakasafirishwa hadi Kakamega

Maafisa wapata ng’ombe kadhaa walioibwa kutoka Nakuru wakasafirishwa hadi Kakamega

Na RICHARD MAOSI

MAAFISA kutoka Kituo cha Polisi cha Kaptembwo, wamefanikiwa kupata sehemu ya mifugo 26 ambayo ilikuwa imeibiwa kutoka Nakuru, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Hii ni baada ya wakazi wa mitaa ya Kaptembwa na Ng’ambo kuwasilisha malalamishi yao kwa maafisa wa usalama, walipotambua mifugo yao – wakiwemo ng’ombe – ilikuwa ikitoweka kwa njia ya utata.

Akizungumza na Taifa Leo, chifu wa Kaptembwo Paul Kirui alisema baadhi ya vijana ambao wamekuwa wakisaka kazi za kulinda mifugo ndio wamekuwa wakiendeleza shughuli hii.

“Wengi wao wamekuwa wakipeleka ng’ombe sehemu za mbali kama vile Mwariki, jambo ambalo sio la kawaida kufanyika hapa,” alieleza.

Isitoshe zaidi ya mara moja, kundi la wachungaji limekuwa likijikuta kwenye mitego ya wezi bila kujua, akisisitiza kuwa ng’ombe 16 ni kutoka kwa mkulima mmoja.

Chifu Kirui alisema uchunguzi wa polisi uliwaelekeza maafisa katika eneo la Kivumbini ambapo inaaminika wezi wamekuwa wakificha, kupakia na kusafirisha mifugo katika miji mingine.

Alieleza kuwa mifugo imekuwa ikipakiwa katika malori kutoka sehemu hii, kisha hatimaye kusafirisha mpaka Kakamega, jambo ambalo baadhi ya wakazi walikiri ni la kweli iapo walitaka tuyabane majina yao.

Mei 28 polisi walifanikiwa kunasa dereva wa lori ambalo lilikuwa limesafirisha mifugo 16 kutoka Nakuru kuelekea Kakamega.

Usiku wa Jumamosi maafisa wa Nakuru walifika Kakamega ambapo walipata ng’ombe saba, ambao hatimaye walirudishwa Nakuru na kuhifadhiwa katika kituo cha Kaptembwo.

“Mpaka sasa polisi wanaendelea kutafuta ng’ombe tisa ambao walisafirishwa baada ya kunasa dereva,” akasema.

Agnes Rono, mkazi wa Ng’ambo alisema ingawa polisi wamefanikiwa kupata baadhi ya mifugo, anataka wafuatilie zaidi ili kurejesha ng’ombe waliosalia.

Alitaka polisi kuwachukulia wezi hatua kali ili kukomesha uovu huu, akiwa mmojawapo wa wale walioathirika baada ya kupoteza mifugo miwili.

You can share this post!

Mbinu mbalimbali za kuimarisha kinga mwilini

Madaraka Dei bila uhuru