Habari za Kitaifa

Maafisa wasaka kichwa cha Rita Waeni

January 18th, 2024 2 min read

BENSON MATHEKA Na PIUS MAUNDU

MAAFISA wa polisi wanaochunguza mauaji ya msichana mwenye umri wa miaka 20 katika chumba cha kukodisha kwa muda mfupi mtaani Roysambu, Nairobi, wanajitahidi kutanzua kitendawili cha kutoweka kwa kichwa chake.

Sehemu za mwili ambao umetambuliwa kama wa Rita Waeni Muendo, mwanafunzi wa chuo kikuu zilipatikana ndani ya chumba hicho karibu na jumba maarufu la kibiashara la TRM, Jumapili iliyopita zikiwa zimepakiwa ndani ya karatasi.

Kulingana na polisi, imebainika kuwa wauaji wa msichana huyo walitumia msumeno kukata mwili wake vipande vipande huku familia yake ikihusisha kisa hicho cha kikatili na utekaji nyara kwa lengo la kudai fidia.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, msemaji wa familia, Dkt Lilian Mutea alisema Waeni alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

“Jumamosi, mtoto wetu Rita Waeni Muendo aliondoka nyumbani kwa shangazi yake mtaani Syokimau, Machakos kwenda kukutana na rafiki yake. Mnamo Jumapili, saa kumi na moja alfajiri, baba yake alipokea ujumbe kutoka kwa nambari yake ya simu, ukiitisha Sh500,000 za kukomboa mateka ndani ya saa 24 ili aweze kuachiliwa,” taarifa ya familia ikasema.

Alisema kwamba familia ilipiga ripoti kwa polisi na uchunguzi ukaanzishwa huku familia ikipokea jumbe mbili zaidi za kuitaka ilipe fidia.

Kinachoshangaza familia ni kuwa waliotuma jumbe hizo hawakuwapa maelezo zaidi au nafasi ya kuweza kuilipa.

“Familia haikupata maelezo zaidi kuhusu fidia hiyo au nafasi ya kuilipa. Zaidi ya hayo, baadhi ya matakwa ya kuilipa yalitolewa akiwa ameuawa tayari,” iliongeza taarifa hiyo.

Alisema familia imehuzunishwa na mauaji ya kikatili ya binti wao.

“Baada ya kutafuta kwa uchungu bila mafanikio, tukishirikiana na DCI, tulimtambua mtoto wetu kuwa msichana aliyeuawa kikatili asubuhi ya Jumapili karibu na Thika Road Mall (TRM), Januari 14. Tunaamini alishawishiwa na muuaji wake, ambaye pia alijaribu kupora pesa kutoka kwa familia yake, hata baada ya kumuua.”

Dkt Mutea alisema familia imevunjika moyo kwa kumpoteza Waeni, na hasa ukatili wa mauaji yake.

“Wazazi wake, ndugu zake, na familia yetu yote bado hatujakubali tukio hilo la kusikitisha. Binti yetu, Waeni, alikuwa msichana mwenye akili na mwerevu kupita umri wake. Alikuwa mtu mwenye roho nzuri na anayejali, anayejulikana kwa ukarimu wake, kicheko, na uwezo kufurahisha kote alikoingia.

Mnamo Jumatano, wapelelezi wanaochunguza mauaji hayo ya kikatili walisema wanawazuilia washukiwa watatu.

Mnamo Jumanne, mwanamume anayeaminika kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya msichana huyo alinaswa katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) alipokuwa akikaribia kuondoka nchini huku ikiibuka kuwa mwathiriwa na aliyemuua walipatana katika mtandao.

Polisi waligundua kuwa nambari ya simu iliyotumiwa kukodisha chumba hicho ilitumiwa eneo la Ruaka siku nne kabla ya mauaji.

Washukiwa wengine wawili walikamatwa na wanaendelea kusaidia polisi katika uchunguzi.

Majirani wa nyumba hiyo ya mauti walihojiwa na wapelelezi, kubaini iwapo walisikia kelele zozote zisizo za kawaida.

Inashukiwa kuwa muuaji alitumia stakabadhi ghushi kusajili laini ya simu kwa jina la marehemu, kisha akaitumia kukodisha chumba hicho ili asigunduliwe.

Polisi wanashuku kuwa waliomuua walimpa mwathiriwa dawa za kulevya kabla ya kuukata mwili wake ndani ya bafu katika chumba hicho.

“Tunashuku kwamba muuaji alimpa mwanamke dawa za kulevya kabla ya kumuua. Hili lilitokea ndani ya bafu ya nyumba hiyo aliyokuwa amepanga,” duru zinazohusika na uchunguzi zilisema.

Kusudi la waliomuua kutoweka na kichwa chake halijabainika.