Maafisa watano wa polisi washtakiwa kwa kumuua mahabusu

Maafisa watano wa polisi washtakiwa kwa kumuua mahabusu

NA RICHARD MUNGUTI

MAAFISA watano wa polisi wameshtakiwa kwa kumuua mahabusu katika kituo cha polisi cha Changamwe.

Khalif Abdullahi Sigat, James Muli Koti, Joseph Odhiambo Sirawa, Edward Kongo Onchonga na Nelson Nkanae walikana walimuua Caleb Otieno akiwa rumande mnamo 2018.

Watano hao walioshtakiwa mbele ya Jaji Momanyi Bwonwong’a wanawakilishwa na Danstan Omari, Cliff Ombeta, Annita Masaki na Samuel Ayora walishtakiwa kumuua Caleb Otieno mnamo Septemba 18, 2018.

Mawakili hao walilalamika kwamba tangu washtakiwa watiwe nguvuni mwaka mmoja uliopita hawakabidhiwa nakala za mashahidi ili waandae tetezi zao.

“Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) haijatukabidhi nakala za ushahidi uliotayarishwa na afisi ya idara ya kuchunguza jinai (DCI) licha ya agizo la hii mahakama washtakiwa wakabidhiwe nakala hizo,” alisema Bw Omari.

Mabw Ayora, Omari na Ombeta walieleza mahakama kuwa mamlaka huru ya polisi (IPOA) iliyochunguza kesi hiyo miaka minne iliyopita imekataa kuwapa maafisa hao wa polisi nakala za uchunguzi wa DCI.

“IPOA inajulikana kwa kutesa polisi. Polisi hutekeleza jukumu muhimu sana kutumikia wananchi. Ni hii mahakama tu inayoweza kuhakikisha haki za maafisa hawa wa polisi zimetekelezwa,” alisema Bw Omari.

Jaji Bwonwong’a alifahamishwa serikali inatakiwa kuwalinda polisi dhidi ya ukiukaji wa haki zao.

Jaji huyo aliamuru IPOA iwakabidhi washtakiwa hao nakala za ushahidi huo.

Mahakama itaamua Oktoba 28, 2022 ikiwa washtakiwa wataachiliwa kwa dhamana.

  • Tags

You can share this post!

Ruto atangaza Baraza la Mawaziri, walioteuliwa sharti...

Japhet Koome ateuliwa awe Inspekta Jenerali wa polisi,...

T L