Habari Mseto

Maafisa watatu wanaswa kwa ufisadi Kaunti ya Samburu

June 15th, 2020 1 min read

NA WAWERU WAIRIMU

Maafisa wa upelelezi wa kukabiliana na ufisadi walikamata maafisa watatu wakuu wa kaunti ya Samburu kwa kutenga Sh8 milioni katika tenda ya kununua trakta Jumatatu.

Watatu hao ni mkuu wa ununuzi Geoffrey Kitewan, mkurugezi mtendaji wa fedha Daniel Nakuo Lenolkirina na mkurugezi mtendaji wa Kilimo Reuben Lemunyete Maruben.

Bw Kitewan alikamatwa Nairobi ambapo alikuwa ametembea wikendi huku wenzake wakikamatwa katika maeneo ya Maralal na Archers Post.

Naibu mkurungezi wa EACC George Ojowi alisema kwamba watatu hao walifeli kuzingatia amri na michakato yza ununuzi kwa kutenga na kuruhusu kampuni ya CMC Motors kulipwa Sh8,418,964 kwa matrakta mawili na plau.

“Walikuwa wamepata kibali cha matrakta sita lakini wakanunua mengine mawili bila kufuata kanuni za ununuzi ,” alisema Ojowi.

Afisa huyo wa EACC alisema kwamba watatu hao watafikishwa kortini hapo kesho na kushtakiwa na mashtaka ya ufisadi.

Alizionya kaunti zinazoshiriki ufisadi kwamba maafisa wake watawakamata wafisadi wote.