Habari Mseto

Maafisa wawili waitwa kortini kuhusu mbolea hatari

April 4th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili katika Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) na Mamlaka ya Bandari (KPA) Alhamisi waliamriwa wafike kortini Aprili 24 kueleza sababu magunia milioni tatu ya mbolea iliyoingizwa nchini Novemba 2017 hayakupimwa madini ya Zebaki kabla ya kutolewa kuuziwa wakulima.

Hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot aliamuru Nicholas Kinoti wa KRA na Abdi Malik (KPA) wafike mahakamani kueleza sababu ya kukaidi agizo mbolea hiyo ipimwe Machi 26/27 2019.

Mahakama ilielezwa na wakili Paul Muite kwamba agizo lake lilikaidiwa na mbolea hiyo haikupimwa.

Pia ilibainika kuwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP imeingiwa na tabia ya kukaidi na kupuuza maagizo ya kortini.

“Naomba mahakama iamuru DPP aeleze sababu maagizo yake hayakutekelezwa,” alisema wakili Ken Nyauncho.

Wakili Ken Nyauncho (kati). Picha/ Richard Munguti

Aliomba maafisa hao wawili waagizwe wafike mahakamani Aprili 24 kueleza sababu za kukaidi maagizo wapime mbole iliyoingizwa nchini Novemba 2017 na kampuni ya OCP (K) Ltd ikiwa iko na madini ya Zebaki.

Awali meneja mkurugenzi wa shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (Kebs) Bw Bernard Nguyo aliahidi kutekeleza agizo hilo kupima mbolea hiyo.

Bw Nguyo aliahidi mahakama kutoa ripoti kortini ya kuhusu ripoti hiyo ya mbolea.

Aliyekuwa MD wa Kebs Bw Charles Ongwae na washukiwa wengine nao wanakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuwaua wakulima kwa kuwauzia mbolea iliyo na madini ya Zebaki.

Kesi dhidi yao itaanza kusikizwa Julai 8, 2019.