Habari

Maafisa wawili wakamatwa huku Sh7m zikipatikana

September 7th, 2019 1 min read

Na AMINA WAKO na MARY WANGARI

KISA cha uvamizi usio wa kawaida kwenye ATM Nairobi ambapo Sh72 milioni ziliibiwa kimechukua mkondo mpya huku wapelelezi kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai wakipata Sh7 milioni.

Mnamo Jumamosi maafisa kutoka Kitengo cha Polisi kuhusu Uhalifu Mahsusi (SCPU) pia wamewakamata maafisa wawili wa polisi.

Kulingana na DCI, Polisi wa Utawala Konstebo Chris Ayienda Machogu amekamatwa akiwa na Sh4 milioni mjini Kisii.

Baada ya kuhojiwa, aliwaongoza makachero hao kwa Konstebo wa polisi Vincent Owour ambapo Sh3 milioni zilipatikana nyumbani kwake Kendu Bay. Wapelelezi hao pia walipata gari.

Mnamo Ijumaa, makachero waliwakamata washukiwa wengine watatu wanaodaiwa kuwa sehemu ya genge lililotoweka na Sh 72 milioni.

Wakati wa kukamatwa huko, wapelelezi pia walipata magari mawili yaliyotumika katika wizi huo.

Kulingana na ripoti ya polisi, gari mojawapo, KCE 920E Voxy, lilipatikana kwenye karakana Kikuyu lilipokuwa likipakwa rangi nyeusi kutoka nyeupe.

Magari yote aina ya Toyota Noah yaliyotumika katika wizi huo yalikuwa yamepelekwa katika karakana ya magari na yalikuwa yamepakwa rangi upya ili kuzuia polisi kuyafuatilia.

Washukiwa hao wamezuiliwa na polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa mwanzo.

Makachero walisema gari lililoopatikana aina ya Subaru Forester nyekundu lilinunuliwa siku ya tukio hilo kwa kutumia hela zilizoibiwa.

Maafisa hao walifichua kwamba washukiwa hao wawili walikuwa wakipanga kusafiri Uganda.