Habari Mseto

Maajabu ya mahindi ya Sh7.6 bilioni kuozea kwa mabohari

November 1st, 2018 2 min read

Na DAVID MWERE

MAGUNIA milioni nne ya mahindi yanayohifadhiwa katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB) ni mabovu na hayafai kuliwa na binadamu wala wanyama.

Kamati ya Seneti inayochunguza sakata ya mahindi nchini Jumatano ilielezwa kwamba mahindi hayo yaligharimu serikali Sh7.6 bilioni.

Kamati hiyo inayosimamiwa na Seneta wa Uasin Gishu, Prof Margaret Kamar, iliambiwa kuwa mahindi hayo ambayo ni sehemu ya magunia milioni sita yaliyonunuliwa Mexico na serikali wakati wa kiangazi mwaka uliopita, sasa yamebadilika rangi ishara ya kuharibika.

Ripoti kuhusu kuharibika kwa mahindi hayo ilitolewa na Idara ya Ubora wa Bidhaa (KEBS) na imetokea wakati ambapo wananchi wengi bado wanatilia shaka usalama wa vyakula baada ya kujulishwa miezi michache iliyopita kwamba sukari nyingi nchini ina sumu.

Wakati huo huo, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, ambaye alifika mbele ya kamati hiyo jana alifichua kuwa magunia milioni 4.4 yaliingizwa nchini kwa njia haramu katika kipindi hicho cha kiangazi mwaka uliopita.

Prof Kamar alimwomba Bw Kiunjuri achukue hatua mara moja kuhusu hali hii la sivyo Wakenya watakuwa hatarini kula chakula chenye sumu.

“Ningefurahi kama NCPB ingechukua hatua kuhusiana na ripoti ya KEBS. Kwa mfano, kile kilichohifadhiwa kwenye maghala Eldoret ni mchanganyiko wa mahindi yaliyonunuliwa kutoka kwa wakulima na yale yaliyoagizwa kutoka mataifa ya kigeni,” akasema Prof Kamar.

Kwenye barua iliyoandikwa kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NCPB, Albin Sang’ mnamo Oktoba 5 mwaka huu, KEBS ilisema majaribio yaliyofanyiwa mahindi yaliyo ghalani kote nchini yalionyesha kuwa ni asilimia 36.7 pekee ya mahindi yalifikia kiwango cha ubora kinachohitajika.

Dkt Henry Rotich ambaye ni mmoja wa mameneja katika KEBS, aliambia kamati ya Seneti kwamba walifanya majaribio kwa sampuli 254 za mahindi kutoka kwa maghala yote lakini ni sampuli 94 pekee zilizofikia kiwango cha ubora kilicho salama kwa lishe ya binadamu.

“Ripoti yetu ni sahihi na hatutaibadilisha. Hii ndiyo hali halisi ya mahindi kwenye maghala kote nchini,” akasema Dkt Rotich.

Lakini Bw Kiunjuri alisema hawezi kutumia ripoti ya KEBS pekee kuamua hatua itakayochukuliwa bali ni lazima asasi nyingine za serikali zijumuishwe kwani suala hilo ni zito mno.

Waziri alisema alisikia kuhusu ripoti hiyo kwa mara ya kwanza jana ilipowasilishwa kwa kamati, lakini Bw Sang akapinga kutoka NCPB alisema aliiwasilisha mapema kwa maafisa katika Wizara ya Kilimo.

Kamati ilipinga wazo la Bw Kiunjuri kuunda jopokazi la uchunguzi, ikisema hatua hiyo itakuwa ni kupoteza muda.