Maajenti wa kazi Uarabuni kuchunguzwa

Maajenti wa kazi Uarabuni kuchunguzwa

NA JURGEN NAMBEKA

SERIKALI imepanga kufanya msako dhidi ya makampuni yanayotafutia Wakenya ajira katika nchi za ughaibuni, hasa zile za Uarabuni.

Kulingana na Waziri wa Leba, Bw Simon Chelugui, Wakenya takriban 97 walifariki kwa njia za kutatanisha nje ya nchi walipoenda kikazi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Akizungumza Jumanne jijini Mombasa, Bw Chelugui alisema Wizara ya Leba ishatengewa Sh70 millioni kwa minajili ya kuandaa nyumba ya kuwahifadhi kwa muda Wakenya wanaojipata katika shida na waajiri wao Saudi Arabia, ili kupunguza mahangaiko yao wanapotaka kurudi Kenya.

Nyumba zaidi aina hiyo zitaundwa katika nchi nyingine ambazo Wakenya huhamia kutafuta kazi.

Akizungumza katika warsha ya waajiri na wanaotafuta kazi, Bw Chelugui alihakikishia wananchi kuwa, serikali ya Kenya inachukulia kwa uzito maslahi ya Wakenya wanaofanya kazi nje ya nchi na itafanya lolote kuwalinda.“Serikali itaweka mikataba na nchi zote ambazo Wakenya wanahamia kutafuta kazi.

Mikataba hiyo itahakikisha nchi husika inawawajibikia Wakenya wanaoingia huko kufanya kazi,” akaeleza.

Aliwataka vijana wote kuhakikisha kampuni inayowasafirisha imesajiliwa na kupewa leseni na Mamlaka ya Ajira nchini (NEA).

“Iwapo mtu atajitokeza na kudai eti anakupeleka kufanya kazi ng’ambo, mchunguze vyema. NEA, imeandaa mtandao wa kuchunguza kama kampuni imesajiliwa. Natumai siku za usoni wizara itaweza kufuatilia kila mmoja anayetoka nchini,” alisema Bw Chelugui.

Kongamano hilo lilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Leba (ILO), Muungano wa kusimamia Uhamiaji (IOM), Shirikisho la Waajiri nchini (FKE) na mashirika mengine.

Taasisi zisizo halali zimekuwa zikilaumiwa kwa miaka mingi kwa kusababisha shida nyingi za Wakenya, ambao wameteseka na kuhangaishwa katika mataifa ya Mashariki ya Kati.

Bi Ida Adel ambaye alikuwa amemwakilisha Msimamamizi wa ILO nchini Uganda, Kenya , Tanzania, Rwanda na Burundi Bw Wellington Chibebe, alieleza kuwa, shirika hilo lilikuwa tayari kuhakikisha Wakenya wanaishi maisha mazuri kila wanapohamia nchi za ughaibuni kufanya kazi.

Mkurugenzi mkuu wa NEA, Bi Edith Okoki alieleza kuwa, Wakenya wengi walihangaika kila waliposafiri kwa kukosa habari kamilifu. Aliongeza kuwa, vijana wengi walikosa kazi kwa kutokuwa na habari, kuhusu wanachotaka waajiri.

Kulingana naye, NEA imejitolea kuwahamasisha ili wapate njia za kupata kazi, ndani na nje ya nchi.

“Shida kubwa tuliyo nayo ni ukosefu wa ajira. Kwa kila wanafunzi 800,000 wanaofuzu kila mwaka, ni 100,000 wanaoajiriwa. Hali hii inawafanya wengi kukata tamaa. Kongamano hili linawaunganisha na waajiri ili msaidike,” alisema Bi Okoki.

Kongamano hilo lilikuwa pia na maonyesho ya kwanza kuwahi kufanyika nchini yanayolenga kuwafunza vijana jinsi ya kutumia mtandao wa NEA, utakaowawezesha kujisajili kama wanaotafuta kazi. Mtandao huo utawasajili waajiri pamoja na kampuni za kibinafsi za kuwaajiri wafanyakazi.

  • Tags

You can share this post!

KIDIJITALI: Apu ya ‘Kalro Garlic’ kusaidia wakulima...

Dadake marehemu Tob Cohen ataka DPP atimuliwe kazini

T L