Habari Mseto

Maandalizi tayari kwa mchezo wa Sarafina Nakuru

September 8th, 2019 1 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

MAANDALIZI ya kuwakaribisha waigizaji wa mchezo maarufu wa Sarafina unaotarajiwa kuandaliwa mjini Nakuru kwa muda wa wiki mbili zijazo, yanaendelea.

Mchezo huo utaigizwa na waigizaji wa humu nchini huku idadi yao kubwa ikiwa ya wale wa kutoka Nakuru.

Uigizaji huo utaandaliwa katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Nakuru kwa siku nne kuanzia Septemba 19 hadi 22.

Kulingana na mkurugenzi wa mchezo huo unaohusisha pia tamasha za nyimbo, Bw Stuart Nash, uigizaji huo unalenga kuwatia moyo waigizaji wa humu nchini haswa wa mashinani na pia kuwahimiza vijana wenye talanta mbalimbali za uigizaji.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukiigiza michezo mingi katika ukumbi wa Nairobi lakini mara hii tunakuja Nakuru ili kukuza vipaji vingi,” alisema mkurugenzi huyo wa ukumbi wa sanaa wa kitaifa Nairobi.

Aliongeza, “Nakuru ni moja wapo ya maeneo ambayo ina vijana wengi wenye talanta mbalimbali ila tu, wengi wanakosa kunawiri kwa sababu hamna yeyote anayewashika mkono.”

Kulingana naye, kaunti ya Nakuru ni baadhi ya maeneo yenye madhari nzuri ya utalii na yanayoweza kutoa nafasi nzuri kwa vijana ambao wanaigiza michezo mbalimbali.

Mchezo wa sarafina ulibuniwa Johanesburg, Afrika Kusini mnamo 1987.Mchezo huo unazungumzia maisha ya mwanafunzi wa shule ya upili katika mazingira ya unyanyasaji na ukabila. Alikuwa na maono ya kuleta mabadiliko miongoni mwa jamii na taifa lake.

Bw Nash pia alitangaza kuwa waigizaji wote watalipwa.