Maandalizi ya Idd yanoga Ramadhan ikifika tamati

Maandalizi ya Idd yanoga Ramadhan ikifika tamati

Na BRIAN OCHARO

MAANDALIZI ya kusherehekea sikukuu ya Idd ul-Fitri yameshika kasi nchini Waislamu wanapojiandaa kukamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Waislamu wanaadhimisha siku kuu hiyo baada ya kutimiza nguzo mojawapo ya dini ya Kiislamu ya kufunga.Hata hivyo, shamra shamra za sherehe hizo hazitakuwa za kawaida kwani wamewekewa kanuni tele zinazonuia kuepusha ueneaji virusi va corona.

Hapo jana, halaiki ya Waislamu waliendelea kufurika kwenye maduka hasa ya nguo, vyakula na masoko kwa maandalizi ya dakika za mwisho ya sherehe hizo.

Bw Bashir Mohamed, muuzaji mbuzi katika soko la Kikowani, Kaunti ya Mombasa, alisema kuwa mifugo hao wamekuwa wachache sana mwaka huu kwani kuna changamoto ya usafirishaji mizigo kutoka Tanzania kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19.

“Covid-19 imetuharibia biashara sana. Mipaka ya Lunga Lunga imefungwa na haturusiwi kuingiza mbuzi Kenya, kwa hivyo wale tulio nao ni wachache mno,” akasema.

“Mbuzi tunao lakini idadi ndogo sana. Watu ni wengi wanaotaka mbuzi na hii inamaanisha lazima bei ipande kidogo. Mimi kawaida huwa nina zaidi ya mbuzi 800 lakini leo niko na 200 pekee,” alisema.

Bw Ahmed Badamana, ambaye alienda kununua mbuzi alilalamika kuwa bei zilikuwa juu sana.“Tunaomba serikali itusaidie ili watu wa kawaida pia waweze kusheherekea siku kuu,” alisema.

Maeneo ya biashara ya Marikiti, Mwembe Kuku, Mwembe Tayari na Maduka makuu ndiyo yaliyovutia wateja wengi kiasi cha kufanya milolongo mikubwa ya magari, tuktuk na bodaboda.

Masoko ya kuuza vyakula yakiwemo Kongowea, Mackinon, Majengo na Majengo ya Sega nayo pia yalikuwa na wateja wengi.Jambo ambalo litawahuzunisha zaidi walio na watoto ni kukosekana kwa sehemu za burudani ambapo watoto hua wanajiburudisha kwa kupanda bembea, na kunywa vinywaji mbalimbali na vyakula vyepesi.

Sehemu hizo za burudani ambazo zitakosekana ni pamoja na uwanja maarufu wa kihistoria wa Makadara na vinginevyo katika maeneo ya Kisauni, Changamwe, Likoni na uwanja wa michezo ya Serani.

Bw Suleiman Hamisi, anayefanya kazi katika duka moja la nguo, alisema kuwa biashara yake imekuwa na faida kubwa kutokana na wateja kuongezeka mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita.

“Tangu mlipuko wa virusi vya corona, hatujawahi kupata biashara nzuri kama ilivyo wakati huu. Tunatarajia kuwa tutaendelea kupata wateja wengi siku ya Iddi,” akasema.

Alisema kuwa wateja wengi wanalalamika kuwa bei zimepanda ghafla na wamewataka wenye biashara wapunguze bei za bidhaa zao kwasababu watu wameumia kimaisha kutokana na janga la korona.

“Hali ya maisha imezidi kuwa ngumu na hivyo wafanyabiashara wanastahili kutufikiria na hasa wale wenzetu Waislamu ambao tumefunga nao saumu kwa mwezi mzima,” alisema Asha Mohamed, mkaazi wa Kisauni, Mombasa.Hata hivyo, mfanyabiashara mmoja alisema kuwa hata wao wameumia kibiashara na wananunua bidhaa hizo kwa bei ya juu.

“Hata sisi hatutaki kuumiza wateja lakini pia hatuwezi kuuza kwa bei duni ambazo zitatutia hasara,” alisema Bw Mustafa Ali anaye uza nguo za wanawake zikiwemo madera na buibui.

You can share this post!

Kenya Power yazidi kumulikwa kwa utepetevu

UEFA: Fainali ya Man City na Chelsea kuandaliwa jijini...