Habari Mseto

Maandalizi ya KCPE, KCSE yakamilika

October 15th, 2019 1 min read

Na DAVID MUCHUNGUH

SERIKALI imetangaza kwamba imejiandaa kikamilifu kuzuia wizi wa mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na wa Kidato cha Nne (KCSE).

Wizara za Elimu, Usalama na Mawasiliano (ICT) zitashirikiana kukabiliana na majaribio ya wizi wa mitihani hiyo.

Akizungumza Jumatatu katika Taasisi ya Mafunzo ya Serikali jijini Nairobi, Waziri wa Elimu George Magoha alisema serikali imeweka mikakati ifaayo kuzuia visa vyovyote vya wizi wa mtihani.

“Karatasi za mtihani hazitaonwa na yeyote, zitaonwa tu na wanafunzi siku ya kufanya mtihani,” akasema Magoha.

Ili kuzuia visa vya wizi wa mitihani, serikali, mnamo 2017 iliamua kutumia masanduku ya chuma yaliyoko katika makao makuu ya kila wilaya.

Kutakuwa na vituo 479 vya kusambaza karatasi za mtihani kote nchini.

Wakuu wa shule ambao ni mameneja wa vituo vya mtihani huchukua karatasi za mtihani kila asubuhi na kuzirejesha jioni.

Wakati wa hafla ya jana, wakurugenzi wa elimu wa wilaya walikabidhiwa funguo za masanduku hayo ya mtihani.

Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alitangaza kuwa idara ya usalama tayari imeandaa vifaa, zikiwemo ndege, kuhakikisha kuwa vituo vya kufanyia mtihani ni salama.

Likizo yafutwa

Dkt Matiang’i pia alifutilia mbali likizo za maafisa wakuu katika idara ya polisi hadi pale mtihani utakapokamilika Novemba.

Aliwaonya wakurugenzi wa elimu wa wilaya dhidi ya kupoteza funguo au vifaa vya mtihani.

“Hakuna ufunguo utapotea na hatutakubali kuwepo kwa kisingizio chochote,” akasema Dkt Matiang’i.

Walimu 179,149 watashirikishwa katika usimamizi wa mtihani huo.

Jumla ya watahiniwa 1,088,987 wanatarajiwa kufanya mtihani wa KCPE utakaofanyika kati ya Oktoba 29 na Oktoba 31, katika vituo 27,809.

Nao watahiniwa 699,746 wanatarajiwa kufanya mtihani wa KCSE utakaong’oa nanga Oktoba 21 hadi Novemba 27 katika vituo 10,896.

Walimu 17 walifutwa kwa kuhusika na wizi wa mtihani mwaka jana.