Habari Mseto

Maandamano: Amerika yatoa tahadhari kwa raia wake


AMERIKA Jumanne ilionya raia wake kuchukua tahadhari ya usalama wakiwa Kenya kutokana na maandamano yaliyopangwa Nairobi.

Katika onyo hili, raia wa Amerika walitakiwa kuepuka maeneo ya kati kati mwa jiji na yanayozunguka majengo ya Bunge.

Wakati huo huo, wakuu wa mashirika ya umma, ambao mashirika yao hayashirikishi umma wakati wa kuunda sera, sheria na bajeti, wanakabiliwa na hatari ya kutozwa faini ya Sh300,000 au kifungo cha miezi sita jela, ikiwa pendekezo lililo mbele ya bunge litaidhinishwa kuwa sheria.

Mswada wa Ushirikishaji Umma, 2023, uliofadhiliwa na Mbunge wa Turkana Magharibi, Bw Daniel Nanok, unalenga kutoa mfumo wa kisheria wa ushirikishwaji wa umma nchini.

“Lengo la Mswada ni kuimarisha, kukuza na kuwezesha ushiriki wa umma katika michakato ya utawala na kuhakikisha michakato yote ya umma kuanzia uundaji wa sera, mchakato wa kutunga sheria na uamuzi wa mwisho unahusisha ushiriki wa watu kikamilifu,” inasema sehemu ya Mswada huo.

Sheria inayopendekezwa inalenga kutoa mfumo wa ushirikishaji umma kwa taasisi za umma ikiwa ni pamoja na bunge, mabunge ya kaunti na serikali za kaunti, ili kupunguza hatari ya kutenga mitazamo na hofu ya umma katika kufanya maamuzi.

“Mtu anayekiuka masharti ya sheria hii anatenda kosa na akipatikana na hatia, ataadhibiwa kwa kulipa faini isiyozidi Sh300,000 au kifungo kisichozidi miezi sita jela au adhabu zote mbili,” unaeleza Mswada huo.

Kabla ya kushirikisha umma, Mswada huo unasema kwamba shirika la Serikali au afisi ya umma litabainisha madhumuni ya ushirikishwaji wa umma, aina ya sheria au uamuzi utakaofanywa.

Mswada huo ulichapishwa kwa mara ya kwanza Septemba 1, 2023, na kusomwa kwa mara ya kwanza Oktoba 12, 2023 na baadaye kupelekwa kwa Kamati ya Bunge ya Utangazaji na Maktaba kuzingatiwa na ripoti kuwasilishwa Bungeni.

Kamati hiyo bado inapitia mapendekezo yaliyo katika Mswada huo na inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake Bungeni.

Kamati tayari imepokea na kupitia mawasilisho kutoka kwa wadau 21 ambao ni; Hazina ya Taifa; Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Usawa; Baraza la Magavana; Kituo cha Utawala wa Kiuchumi na mashirika kadhaa ya kiraia na yasiyo ya kiserikali.

Ripoti zaidi na Eric Matara