Habari za Kitaifa

Maandamano: Barabara karibu na Ikulu zafungwa

Na BENSON MATHEKA June 27th, 2024 1 min read

POLISI wa kupambana na ghasia wamefunga barabara karibu na Ikulu ya Nairobi katika juhudi za kuwazuia waandamanaji ambao wameapa kuendelea na maandamano licha Rais William Ruto kuondoa Mswada tata wa Fedha 2024.

Polisi wanawazuia baadhi ya madereva na watu waliotembea kwa miguu wanaotumia barabara hizo.

Waandamanaji waliapa kuendelea na maandamano kulaani hatua ya Bunge kupitisha Mswada wa Fedha wa 2024.

Rais William Ruto alikataa kutia saini mswada huo na kuwataka Wabunge kufuta vipengee vyote vilivyomo.

Barabara zilizoathirika ni pamoja na Dennis Pritt, State House Avenue, Processional Way, Valley Road, Jakaya Kikwete Road na zinazoungana nazo.

Waliwataka madereva wa magari na watembea kwa miguu kujitambulisha na dhamira yao kuwa karibu na Ikulu.

Wale wanaoishi karibu walitakiwa kukaa ndani au kuondoka na kurudi jioni, walisema.

Polisi pia wanashika doria katikati mwa jiji na barabara kuu zinazoelekea jijini kabla ya maandamano yaliyopangwa.

Waandamanaji hao walisema walipanga kuandamana hadi katikati mwa jiji kuomboleza waliouawa katika maandamano yaliyopita yakiwemo ya Jumanne walipovamia majengo ya Bunge.

Biashara nyingi  zimefungwa na kuna magari machache.

Polisi waliwahakikishia waliofungua biashara zao usalama wao.

Ripoti zinaonyesha polisi zaidi wa kupambana na ghasia walitumwa katika miji mikubwa nchini kabla ya maandamano yanayotarajiwa.

Vizuizi zaidi viliwekwa kwenye barabara karibu na ikulu ndogo za serikali.