Habari Mseto

Maandamano holela hayawasaidii nyinyi vijana – Ali Mbogo

July 19th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kisauni Ali Mbogo amewaonya vijana kutoka Kaunti ya Mombasa dhidi ya kutumiwa ‘vibaya’ na wanasiasa.

Aidha alisema vijana wanafaa kujishughulisha na njia za kuimarisha maisha yao badala ya kujihusisha na maandamano.

“Msikubali kutumiwa na watu wenye nia mbaya kufanya maandamano. Mnapewa pesa halafu mnamiminika barabarani kuandamana; hiyo haifai kabisa,” alisema Bw Mbogo.

Bw Mbogo ambaye alishatangaza azma yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa alisema vijana kadhaa waliandamana hivi majuzi kutokana na swala la barabara katika eneobunge lake.

“Ni umbali wa kilomita chache tu unaobakia ili barabara ikamilishwe lakini mmedanganywa mkaandamana. Changamoto ya barabara hii si mkandarasi bali serikali ambayo haijamaliza kumlipa fedha zake. Kwa nini watu hawaoni kilomita 12 ambazo zimekamilika tayari na iko hali nzuri sana? Kwanza nilipochaguliwa kuwa mbunge nilijizatiti kuhakikisha ujenzi wa barabara hii unazingatiwa,” alisema Bw Mbogo.

Alisema eneobunge lake lina barabara bora zaidi akisifu uongozi wake ambao umeleta maendeleo Kisauni.

Bw Mbogo alisema anapigwa vita sababu ametangaza kuwa anataka kuwania kiti hicho cha ugavana mwaka 2022.

“Kuna sehemu wilayani Mvita ambapo kuna barabara mbovu sana lakini watu wanaona hapa Kisauni tu! Mimi si msaliti, ni tishio la wagombea wengine wa ugavana,” aliongeza.