Habari za Kaunti

Maandamano Kiganjo kupinga ‘udhalimu’ wa kanjo wa Kiambu

April 23rd, 2024 2 min read

NA LAWRENCE ONGARO

WAFANYABIASHARA na wanakijiji cha Kiganjo wapatao 1,000 waliandamana Jumatatu wakidai wananyanyaswa na askari (kanjo) wa Kaunti ya Kiambu.

Walidai kuwa ada za leseni zimepandishwa maradufu na kanjo wanatumia ukatili kutekeza amri, sheria na sera.

Waandamanaji walidai kuwa mtaa wa Kiganjo ambao una takriban wakazi 50,000 na uko mjini Thika, hauna huduma kamili za kimsingi lakini kanjo wa Kaunti ya Kiambu wamekuwa kero kwao.

Walisema wanahangaishwa kuhusu leseni za biashara.

Licha ya wao kulipa ada hizo, walidai barabara ni mbovu, hakuna kituo maalum cha magari na kwamba majitaka yametapakaa kila mahali.

Pia walisema wanakosa hospitali maalum katika eneo hilo.

Mfanyabiashara kutoka Kiganjo akiandamana Aprili 22, 2024, kulalamikia kile alidai ni kunyanyaswa na askari (kanjo) wa Kaunti ya Kiambu. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mfanyabiashara Mburu Ngugi ambaye ni mhudumu wa M-Pesa na vifaa vya kielektroniki, alisema wataanza kukusanya saini za wakazi wa Kiganjo ili kumlazimisha Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi kusikiliza kilio chao.

“Tumevumilia vya kutosha na hatutakubali askari wa Kaunti ya Kiambu kutuhangaisha kiholela,” alisema Bw Ngugi.

Mwenzake, Bi Milka Wahome, alisema Kiganjo imekuwa na wakazi wengi na kwa hivyo ni vyema kupata huduma zifaazo.

Alilaani hatua ya kanjo hao kuwahangaisha wafanyabiashara kila mara.

“Askari hao hawana utu kwa sababu wao huingia ndani ya maduka na mikahawa kwa fujo na kuchukua mali zetu huku wakitutolea vitisho,” alisema Bi Wahome.

Bw Boniface ‘Wanjoki’ Kabugu alidai kuwa Kaunti ya Kiambu imewafinya wafanyabiashara kwa kuwatoza kodi za juu kupindukia.

Alisema hata wafanyabiashara wanaouza bidhaa tofauti kama vyuma na mbao wanalazimika kukata leseni na kibali cha afya.

Soma Pia: ‘Ufisadi wa polisi, kanjo utaponza Thika kuwa jiji’

Alisema kaunti hiyo haijawapa huduma ya kuridhisha.

Naye Bi Lucy Njeri alilalamika hali mbovu kwa kukosekana huduma za afya na vyoo safi na salama katika maeneo ya biashara.

“Hapa Kiganjo hatuna hata hospitali ya kuhudumia wakazi wa hapa. Mvua inaleta kero ya mafuriko katika eneo lote hili,” alisema Bi Njeri.

Bi Jane Gathoni ambaye huuza aiskrimu, alisema alitozwa ada ya Sh18,000 kwa mwaka badala ya Sh9,000 za hapo awali.

Alisema biashara hiyo imeanza kuwa ngumu kwake kwa sababu hata wateja wamepungua.

Malalamiko hayo yanajiri huku mchakato wa kufanya Thika kuwa jiji ukishika kasi.