Habari

Maandamano kupinga wanafunzi kupewa kondomu yanukia

February 20th, 2019 1 min read

NA TITUS OMINDE

BARAZA la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) eneo la North Rift limetishia kuandaa maandamano  kupinga mipango ya serikali ya kuwapa wanafunzi kondomu.

Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Abubakar Bin Jumatano aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa mipango ya serikali ya kuwapa wanafunzi wa shule za upili na vyuo kondomu kama njia moja ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni ukosefu wa maadili.

Sheikh Bin alisema kusambazia wanafunzi kondomu na sawa na kuidhinisha usherati na ukosefu wa maadili miongoni mwa wanafunzi.

“Sisi kama Waislamu kamwe hatuungi mkono mpango wa Baraza la Kitiafa la Kupambana na Ukimwi nchini (NACC) wa kuwapa wanafunzi kondomu, mpango kama huu unaashiria upotovu wa maadili na kukosa kumheshimu Mungu,” alisema Bin

Bw Bin alitilia mkazo umuhimu wa kuimarisha kampeni ya kuwataka wanafunzi kujiepusha na mapenzi kiholela, huku akitaka serikali kuendeleza kampeni ya kuwataka wanafunzi kujiepusha na ngono hadi pale watakapoingia katika ndoa.

Kiongozi huyo alitaka serikali kutoa fedha zaidi kwa Baraza la NACC ili kuimarisha kampeini dhidi ya Ukimwi kwa kushirikiana na wadau wengine.

“Iwapo serikali inajali afya ya Wakenya ni sharti taasisi muhimu kama NACC kupewa fedha za kutosha kupambana na maambukizi ya virusi vya HIV,” alisema Bin.

Baraza hilo limeonya Wizara ya Elimu dhidi ya kuwapa wanafunzi kondomu ambapo viongozi wa baraza hilo wamesema wataanza kushiriki maandamano kila Ijumaa kupinga pendekezo hilo iwapo serikali haitasikia ushauri wa dini kuhusu mpango huo.

Mapema wiki hii Naibu Mkurugenzi wa NACC Bw John Kimigwi alitangaza mipango ya baraza hilo kuanza kusambaza kondomu shuleni ili kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya Ukimwi miongoni mwa vijana.