Habari Mseto

Maandamano kuwashinikiza UhuRuto kuweka lami barabara

September 17th, 2018 1 min read

Na VITALIS KIMUTAI

SHUGHULI za uchukuzi zilikatizwa kwa muda saa tano mnamo Jumamosi katika barabara ya Kyogong-Sigor-Chebunyo, Kaunti ya Bomet wakazi wakiishinikiza serikali kuitengeneza.

Wakazi walilalama kwamba Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto waliahidi kuiweka lami kwenye kampeni zao mwaka uliopita, ila hilo halijatimizwa hadi sasa. Barabara hiyo ni ya kilomita 35.

Walisema kuwa viongozi hao wametoa ahadi hizo mara mbili-mnamo 2012 na 2017, ila wangali kuitimiza hadi sasa.

Wanasema kuwa ukarabati wake ndiyo njia ya pekee utakaorahisisha shughuli za uchukuzi katika eneobunge la Chepalungu.

“Ni masikitiko kwamba serikali ya kitaifa imekosa kutimiza ahadi yake, licha Rais Kenyatta kuahidi mara kadhaa kwamba ingejumuishwa katika ajenda ya maendeleo ya serikali,” akasema Bw Victor Koech, kiongozi wa vijana ambaye aliongoza maandamano hayo.

“Wakazi wameteseka sana kwa miaka mingi kwani hukumbwa na changamoto nyingi wanaposafirisha mazao yao, huku watu wagonjwa wakikumbwa na ugumu kufikia huduma bora za afya haraka,” akasema Bw Koech.

Akaongeza: “Akina mama wajawazito hulazimika kusafirishwa hospitalini kwa pikipiki, ambapo baadhi yao huwa wanajifungulia barabarani. Baadhi yao hata wamefariki kwa kuzidiwa na hali zao.”

Hata hivyo, mbunge wa eneo hilo,Bw Gideon Koskei alikosoa maandamano hayo, akisema hayafai, kwani washiriki wangeshauriana na viongozi wao ili kubaini hali ilivyo.

“Nimewaambia wakazi mara kadhaa kwamba nimeshauriana na Bw Ruto, ambapo ameniahidi kwamba fedha zimetengwa katika Bajeti ya Mwaka 2018/2019,” akasema.