Habari za Kitaifa

Maandamano ya amani yalivyogeuka kuwa wizi wa kushtua

Na FRIDAH OKACHI June 27th, 2024 2 min read

WAFANYABIASHARA mbalimbali jijini Nairobi wanakadiria hasara kubwa baada ya maduka yao kuvamiwa na mengine kuchomwa wakati wa maandamano ya Jumanne Juni 25, 2024, yaliyolenga kuwashinikiza wabunge kutupilia mbali Mswada wa Fedha wa 2024.

Katika eneo la Bus Station barabara ya Mfangano, jumba la Sunbeam liliteketea baada ya vijana waliokuwa wakifanya maandamano kulitia moto.

Mfanyabiashara Micheal Ndung’u aliambia Taifa Dijitali jumba hilo liliteketezwa na vijana waliokuwa wakiandamana baada ya jiwe kutoka juu kuangukia mwenzao kwenye kichwa na kumpelekea kufariki.

Bw Ndung’u alisema tukio hilo lilifanyika mwendo wa saa kumi na mbili jioni, wakati wafanyabiashara hao walipokuwa wakifunga maduka yao.

Hali ya mshikeshike ilipozidi, wafanyabiashara hao waliacha milango wazi.

“Haya maandamano hapana, tumeathirika sana wale wenye tuko na biashara kwenye barabara hii,” alilalamika Bw Ndung’u.

“Mwanzo tulikuwa vizuri, hatukujua kuna jinsi moto ungetokea. Ghafla, maGen Z walikuwa wanapita na kwa bahati mbaya kuna jiwe lilirushwa kutoka juu na kugonga mwenzao akaanguka akafa. Wakati wa tukio hilo, vijana hao walisema mbona wamepiga mwenzao na jiwe,” alieleza Bw Ndung’u.

Duka la televisheni, meko na simu lilivyoibwa. Picha|Fridah Okachi

Hata hivyo, vijana hao waliteketeza jumba hilo ambalo lina zaidi ya maduka 100 ambayo hutumiwa kwa biashara mbalimbali.

Waandamanaji hao walijawa na hamaki punde tu mwenzao alipokata roho na kuanza kuchoma maduka mengine.

Katika barabara ya Kimathi, jumba la Old Mutual, duka la Anisuma ambalo lilikuwa likiuza televisheni, meko ya kupika, simu pia yalivujwa.

Msimamizi wa duka hilo Bw Dennis Karanja alisema wamepata hasara ya zaidi ya Sh10 milioni.

“Hatujaweza kuokoa chochote, asubuhi ya leo tumepata boksi tupu. Kulingana na mlinzi wetu, vijana hao walimzidi na hivyo walianza kubomoa na kubeba. Maafisa wa polisi kwa wakati huo hawakuweza kufika ili kuweka ulinzi,” alisema Bw Karanja.

Wakati huo wa maandamano, maduka ya Naivas na Carrefour kando ya ukumbi wa jiji pia yaliharibiwa na kuporwa wakati wa maandamano.

Jengo la nyumba ya Uganda lilipigwa kwa mawe na baadaye kuchomwa moto wakati wa maandamano hayo.