Maandamano ya wakazi kupinga kanisa ‘kunyakua’ shamba

Maandamano ya wakazi kupinga kanisa ‘kunyakua’ shamba

Na PETER MBURU

MAKUMI ya wakazi wa kijiji kimoja kutoka eneo la Subukia kaunti ya Nakuru Jumapili walitekeleza maandamano ya amani, wakilalamikia hali ya kanisa moja kukatalia shamba lao, hali ambayo walisema imewasababishia mateso.

Wakazi wa kijiji cha Ime, wakiongozwa na wazee wakongwe walilalamika kuwa usimamizi wa kanisa la AIC umenyakua shamba lao la ukubwa wa ekari nne, sasa wakitaka serikali kuingilia kati.

Wakazi hao walieleza wanahabari kuwa takriban miaka 20 iliyopita, walitenga shamba hilo, kati ya shamba walilomiliki kwa jumla likiwa ekari 1,500 na kulipa kanisa hilo, kwa maelewano kuwa lingejengwa kanisa na kituo cha afya, kisha kanisa kuhakikisha kuwa kituo hicho kinawatolea watu huduma za afya.

Hata hivyo, wakazi walisema kuwa baadaye kanisa lilishindwa kuendesha kituo hicho cha afya, jambo ambalo sasa limewapelekea wakazi kutafuta huduma za matibabu hadi umbali wa kilomita 12, wengi wao wakiwa wazee wakongwe ambao wanaugua mara kwa mara.

“Tuliamini kanisa kwa kuwa hatukudhani kuwa lingetufanyia hivi, lakini sasa hali imegeuka kuwa mateso tupu na tunapolitaka kanisa kuturejeshea shamba kwa kuwa halikutimiza maelewano yetu, wasimamizi wanakataa,” akasema Bi Mary Wanjiru, mmoja wa wakazi waliokuwa wakiandamana.

Wakazi hao sasa walisema wanalitaka kanisa kuwarejeshea shamba lao ili waipe serikali, ndipo iweze kuijenga kifaa cha afya na kukisambazia dawa na wahudumu wa afya ambao watasaidia.

Japo tayari wanadai kuwa wamefanya kikao na serikali ya kaunti ya Nakuru na kuelewana isimamie kifaa hicho cha afya, wakazi wanasema kuwa serikali ilikataa kukipa dawa wala wahudumu, kwa kuwa kwa sasa shamba hilo linamilikiwa na kanisa.

Wakazi hao walisema wamekuwa wakijaribu juhudi za kulitaka kanisa kuwarejeshea hati ya umiliki wa ardhi hiyo, japo wasimamizi wanapiga chenga.

“Ni mtoto wetu anayesimamia kanisa hilo, na tulipowapa shamba tuliamini tungepata suluhu ya matatizo ya maji na kiafya, lakini sasa hatujapata. Hatutaki watoto wetu kuendelea kuteseka, ilhali tulijitolea ili tusaidike sote,” akasema Bw George Kinuthia.

Wakati wa maandamano hayo, kikosi kikubwa cha polisi kilitumwa karibu na kituo hicho cha afya na kanisa la AIC, la eneo la Ime, kwa hofu kuwa maandamano ya wakazi hao yangegeuka kuwa ya fujo na kuvuruga ibada.

Hata hivyo, wakazi walibeba matawi na kuzunguka shamba hilo wakiimba tu na kukariri kuwa wanataka shamba lao lirejeshwe, bila vurugu yoyote.

Aidha, kwa umoja na kuonyesha namna hawataki kanisa kuendelea kusimamia kifaa hicho, walilifuta jina AIC Ime dispensary kwenye kifaa cha afya kwa rangi na kukariri kuwa wamechoka kuteseka.

Mhubiri wa kanisa hilo la AIC, hata hivyo, alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mzozo huo, akielekeza kwa mkubwa wake, Reverend John Kirogo anayesimamia AIC eneo la Nakuru Kaskazini.

Bw Kirogo alikiri kuwa kanisa lilipewas shamba hilo bure na wakazi na kuendelea kusema kuwa baada ya muda lilishindwa kusimamia, japo akikosa uwazi kuhusu ikiwa kanisa liko tayari kuwarejeshea wakazi hati ya umiliki wa ardhi.

“Tulifanya mikutano na wakazi na wakakubali kutupa shamba hilo, hata hivyo, tulikuwa tumejaribu kushirikiana na serikali ya kaunti ili itupe wahudumu wa afya na dawa japo bado hatujafanikiwa,” akasema Bw Kirogo.

‘Sina uwezo’

Mhubiri huyo aidha aliendelea kusema kuwa ili wakazi warejeshewe shamba hilo, itabidi wasimamizi wa kitaifa wa kanisa kuamrisha, akisema yeye hana uwezo wa kufanya hivyo.

“Ninaruhusiwa kutafutia kanisa mashamba lakini sina nguvu za kuwarejeshea hati ya umiliki ardhi, kunaye msimamizi wa idara hiyo Kenya ambaye wanafaa kumfikia,” akasema.

Lakini wakazi wanalalamika kuwa japo lilipopewa shamba ilikuwa katika maelwano ya Amani, kanisa sasa linajaribu kupiga chenga na kukatalia shamba lao.

Wakazi sasa wanawaomba viongozi wa kisiasa kuingilia kati ili kuhakikisha kuwa mzozo huo ambao ulianza mnamo 2013 unamalizwa, ili waanze kupata huduma walizotaka, wakati walipokuja pamoja.

Wazee wa kijiji hicho walisema kuwa juhudi za kutafuta kikao na wasimamizi wa kanisa zimekuwa zikigonga mwamba, japo nao wasimamizi wakidai kuwa kunao viongozi wa kisiasa wanaowatumia wakazi kulalamika.

You can share this post!

TAHARIRI: Polisi mpakani wachunguzwe

Kiongozi wa wasiomwamini Mungu asimamishwa kazi

adminleo