Habari MsetoSiasa

Maangi adai maisha yake yamo hatarini

January 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU GAVANA wa Kisii Joash Maangi sasa anadai maisha yake yamo hatarini saa chache baada ya watu waliodai kuwa maafisa wa polisi kuvamia boma lake kutwaa magari yake rasmi.

Alitoa madai hayo huku mkutano wa kutoa uhamasisho kuhusu mapendekezo yaliyoko kwenye ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) ukianza mjini Kisii, shughuli ambao Bw Maangi ameupinga akiitaja kama “njama ya kufuja pesa za umma.”

“Mwendo wa saa kumi alfajiri leo (jana) takriban maafisa 12 walifika nyumbani kwangu mjini wakiwa na mitambo ya kuburuta magari niliyopewa na serikali ya kaunti lakini wafanyakazi wangu wakawapa vifunguu na watatwaa magari hayo,” akawaambia wanahabari mjini Kisii.

“Sasa nahisi kuwa maisha yangu yamo hatarini kwa sababu mnamo Jumatatu usiku, gari lenye nambari ya usajili ya serikali ilinifuata nikisafiri kutoka Nairobi kwenda Kisii. Lakini nililikwepa kwa kubadili barabara,” Bw Maangi akaongeza.

Na kwenye ujumbe aliyoandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook Naibu huyo wa Gavana alikariri kuwa kuna watu fulani wanaotaka kumwangamiza ili kuzima ndoto yake ya kuwania ugavana wa Kisii 2022.

“Kwa kufuatwa na watu nisiowafahamu wiki hii na baada ya kitendo cha leo ambapo nilipokonywa magari yote, nahisi kuwa maisha yangu yamo hatarini. Nawaomba Wakenya waniombee,” akasema Bw Maangi ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto.

Mnamo Jumanne wiki hii, Bw Maangi alipinga mkutano wa BBI ulifanyika jana mjini Kisii akisema umepangwa na viongozi waliodai ni wafisadi “ili kuendeleza wizi na ubadhirifu wa pesa za umma.”

Alisema mkutano huo haukuwa na ajenda zozote zenye manufaa kwa wakazi wa kaunti ya Kisii na eneo la Nyanza kwa ujumla.

Na mnamo Januari 2 Bw Maangi alimwonya Waziri wa Usalama Fred Matiang’I dhidi ya kutangamana na viongozi fulani kutoka eneo la Gusii aliodai ni wafisadi.