Makala

AKILIMALI: Mpishi hodari akiri ufugaji wa ng'ombe umemtuliza kifedha

November 7th, 2019 3 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

SAMMY Ng’etich anakumbuka jinsi alivyoenzi upishi.

Alikuwa amehitimu katika masuala hayo na aliyafurahia sana.

Baada ya kukamilisha kozi yake ya masuala ya upishi katika chuo cha Kenya Utalii, Ng’etich alitambua kuwa kuandaa mapochopocho na kubuni mbinu mpya za upishi bora ndio kazi ambayo ingemfaa maishani.

Hata hivyo, mwaka wa 2011 hali ilibadilika huku tasnia ya hotelini ikionekana kukosa kumfaa tena.

“Ushindani kwenye tasnia ya hotelini ina kishindo. Na usipojipanga sawasawa, utabaki kuwa maskini siku zote. Niliajiriwa kazi kwa miaka mingi lakini sikuweza kujikimu maishani.

Kila niliporauka kufika kazini, moyoni mwangu nilihisi kuwa nateseka,” anaeleza.

Hapo ndipo moyo ulimuelekeza kwa kilimo cha mahindi nyumbani kwao katika eneo la Rongai, kaunti ya Nakuru.

Ng’etich alipanda mahindi kwa mara ya kwanza kwenye shamba la ekari moja na kisha akavuna magunia 18 ya bidhaa hiyo.

“Nilikaa kwa muda na mahindi hayo bila kupata soko na nikalazimika kuyauza kwa madalali ambao walinunua kwa bei duni mno,” anaongeza.

Anaeleza kuwa alipata Sh20,000 pekee pesa ambazo aliamua kununua ng’ombe mdogo aina ya Friesian.

“Sikukata tamaa licha ya kipato kidogo nilichopata kutokana na kilimo cha mahindi. Nilitamani kufuga ng’ombe wa maziwa hata ingawa sikuwa na uzoefu wake,” anaeleza.

Mwaka uliofuata, Ng’etich alisema kuwa aliendelea na kilimo cha mahindi kilichomwezesha kupata mapato sawia na yale ya kwanza na akaongeza ng’ombe mwingine.

“Haikuwa rahisi kwangu, nilipata changamoto kubwa sana kuwakuza ng’ombe hao. Mara kwa mara sikufahamu aina ya chakula wala dawa ambayo nilifaa kuwapa,” anasema.

Kwa sababu ya kujitolea na kuwa na ari ya kutaka kujiendeleza kimaisha, alianza kuwatafuta wataalamu wa mifugo waliomwelekeza na kumsajili ili awe akihudhuria mikutano yao kwa manufaa ya kilimo chake kipya.

“Nilifaidika sana na kujihisi kuwa sikukosea kujitosa katika kilimo hiki. Ng’ombe wangu walionekana kuongeza kiwango cha maziwa walichokuwa wakinipa kutoka lita 10 hadi zaidi ya lita 25,” anaeleza kwa tabasamu.

Kilichomwezesha kufikia malego yake anasema ni uvumilivu na kuwa na ari ya kutaka kujifunza mambo ambayo hakuyafahamu.

Mnamo mwaka wa 2014, alipokea mafunzo kuhusu jinsi ya kuboresha kizazi cha ng’ombe wake kupitia uvumbuzi wa teknolojia, uundaji wa malisho na uhifadhi na pia kuongeza thamani ya bidhaa.

Kujiunga na wakulima na wafugaji

Anaeleza kuwa mikutano ya mafunzo ya wataalamu imemwezesha pia kujiunga na wakulima na wafugaji wengine ambao wako katika makundi mbalimbali ya maendeleo.

“Kwa wakati huu nina ujuzi wa kutengeneza chakula cha kutosha wakati wa msimu wa mvua na kisha kukihifadhi hadi wakati wa kiangazi. Kila ng’ombe anastahili kulishwa kiwango fulani cha chakula kila siku,” anasema.

Jambo hilo limemwezesha kudumisha kiwango cha maziwa anachopata kutoka kwa kila ng’ombe.

“Kiwango cha maziwa cha wakati wa mvua kimebakia kuwa kile kile hata wakati wa msimu wa jua kwa sababu nimekuwa nikifuata maelekezo ya wataalamu bila kupuuza,” anasema. Kiwango hicho kimebaki kuwa kati ya lita 20 hadi 25 kutoka kwa kila ng’ombe.

Kwenye ghala lake, ameweza kuhifadhi mabua kavu ya mahindi, nyasi na vyakula vyinginevyo kwa viwango vikubwa.

Pia kando ya ghala hilo kuna tangi kubwa ambalo limejengwa chini ya ardhi lenye uwezo wa kuhifadhi takribani lita 110, 000 za maji.

“Maji haya huwasaidia ng’ombe wangu wakati wa kiangazi. Sina shaka kwani hata wakati hamna mvua ya kutosha ng’ombe wangu hawaathiriki kwa kushusha kiwango cha maziwa wanachonipa kila mwaka,” anasema.

Akilinganisha kilimo cha mahindi na ng’ombe wa maziwa, Ngetich anasema kuwa maziwa yana faida kubwa iwapo mfugaji wa ng’ombe atazingatia ushauri wa wataalamu.

“Mkulima wa mahindi ana uwezo wa kupata Sh36,000 pekee kutoka kwa mazao ya shamba la ekari moja kwa mwaka mmoja, ikizingatiwa kuwa mahindi huchukua takribani miezi 10 shambani. Na akiwa anafuga ng’ombe watano hivi, faida yake ni kubwa,” anaeleza.

Anaongeza kuwa, ng’ombe watano wenye uwezo wa kutoa lita 20 kila mmoja, watampa mfugaji zaidi ya Sh500,000 kwa mwaka.

Kulingana na mfugaji huyo, kwa sasa yuko sawa kifedha kwani uzalishaji wa maziwa umemfanya kuwa huru ikilinganishwa na kazi ya kuajiriwa.