Makala

MAARIFA YA KILIMO: Mvua, mafuriko yatakuponza zao la nyanya, ila hii mbinu itakuokoa

October 31st, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

IWAPO umezuru masoko katika siku za hivi punde, utagundua kuwa zao la nyanya limesheheni, wateja waraibu wa kiungo hiki cha mapishi wakitaja bei wanayouziwa kama nafuu ikilinganishwa na wakati mfumuko unashuhudiwa.

Kifungu cha nyanya tatu au nne za wastani kinagharimu Sh10, hata ingawa kuna kubwa zinazouzwa tatu Sh20.

Kwenye uchunguzi wa Akilimali, baadhi ya wafanyabiashara wanaishia kutupa zingine, hasa zinapooza.

Aghalabu, nyanya zinazodumu muda mrefu ni siku saba pekee, chini ya kiwango cha joto la kadri.

Kwa kuwa hawana njia mbadala kuhifadhi zao hilo kama vile kwa kutumia jokofu, wanalazimika kustahimili mjeledi wa hasara. Hali hiyo ni sawa na inayowakumba wakulima wenyewe wa nyanya.

Isemwavyo mkuki kwa nguruwe mtamu ila kwa binadamu mchungu, wakulima ndio wamelemewa zaidi na pigo hilo kwa sababu zinaozea shambani.

“Hasa mwezi Agosti na Septemba, hatukuwa na budi ila kuruhusu ziozee shambani, bei nayo ilikuwa duni,” Charles Wamae, mkulima kutoka Kirinyaga akalalamika wakati wa mahojiano. Kreti ya kilo 75 kwa sasa inagharimu Sh4, 900. Bei ya nyanya haitabiriki, na hutegemea misimu.

Zao hilo kuozea shambani pia linachangiwa na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa maeneo mbalimbali nchini, barabara za kuingia mashinani zikikosa kupitika.

Ili kutatua baadhi ya changamoto hizo, wakulima wanashauriwa kukuza nyanya zinazohifadhika kwa muda mrefu, zaidi ya siku saba. Baadhi ya kampuni au mashirika yanayounda pembejeo, haswa mbegu, wametafiti na kuibuka na nyanya za aina hiyo.

“Mbali na kuangazia suala la kuoza haraka, nyanya zinazodumu muda mrefu zinasaidia kudhibiti mfumuko wa bei upungufu unapoanza kushuhudiwa,” asema Caroline Murage, kutoka Safari Seeds, mojawapo ya kampuni zinazotengeneza mbegu za nyanya, mboga na maboga, miongoni mwa mazao mengine.

Kulingana na mtaalamu huyo, haja ipo kwa wakulima kuzingatia mbegu zinazostahimili magonjwa ibuka hasa msimu wa mvua na baridi. Nyanya huathirika zaidi na magonjwa wakati wa mvua kubwa, nao wadudu wakishuhudiwa msimu wa kiangazi, wakitafuta lishe.

Kwa mfano, Safari Seeds imeibuka na nyanya aina ya President F1 na kwa mujibu wa maelezo ya Caroline ina sifa zinazoipa ustahimilivu katika maeneo baridi na yenye joto kali. Aidha, mazao yake yanadumu karibu siku 21 baada ya kuvunwa.

“Hata ingawa nyanya hazikosi changamoto za magonjwa na wadudu, chaguo la aina ya nyanya linaambatana na ufanisi katika kilimo chake,” aelezea afisa huyo.

Mbegu bandia

Masoko yamesheheni mbegu bandia, na himizo la mdau Caroline kwa wakulima ni wawe makini na waangalifu wanaponunua. Isitoshe, nyanya zinazodumu muda mrefu zitampa mkulima wakati murwa kutafuta soko bora.

Nyanya ni miongoni mwa mazao yaliyovamiwa na mawakala na madalali. Wafanyabiashara hao wameshika mateka bei, mkulima na mteja mlaji wakiishia kupunjwa.

Ikiwa bei hairidhishi, mkulima anahimizwa kuwa na njia mbadala kutafutia mazao yake soko. Mfano, kuna uongezaji wa thamani, ambapo anaweza kutengeneza bidhaa zitokanazo na nyanya kama vile tomato sauce.

Japo huo ni uwekezaji unaohitaji maelfu au mamilioni ya pesa, wakulima wanaweza kuungana kwa makundi, wachange mtaji wa kununua mashine za shughuli hiyo. Pia ni rahisi kwa makundi kupata mkopo wa vyama vya ushirika (Sacco) au mashirika ya kifedha.