Habari Mseto

Maaskofu wa kanisa Katoliki wataka Jubilee ikomeshe mivutano baina ya viongozi

May 24th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MASKOFU wa Kanisa Katoliki nchini Jumapili wamekemea malumbano ya kisiasa yanayoendelea ndani ya chama tawala Jubilee wakati huu ambapo taifa linakumbwa na changamoto nyingi.

Kwenye taarifa iliyotolewa na Askofu wa Dayosisi ya Eldoret Dominic Kimengich, maskofu hao chini ya Mwavuli wa Muungano wa Maskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB) wamewataka wanasiasa wakomeshe siasa na kuelekeza nguvu katika maswala yatakayowafaa raia wanaopitia hali ngumu.

Askofu Kimengich alisema siasa za migawanyiko zinaweza kutumbukiza taifa hili katika lindi la machafuko.

“Watu wetu wamechanganyikiwa na hawaelewi kinachoendelea baina ya wanasiasa wetu. Wameshindwa kuelewa ikiwa wajibu wa wanasiasa ni kutekeleza ahadi walizowapa wananchi au ni wao wenyewe kufarakana mara kwa mara,” akasema Askofu Kimengich.

“Watu bado wanaumia, baadhi yao bado wana makovu ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007. Wanasiasa hawafai kuturejesha katika enzi hizo,” akaongeza.

Joto la kisiasa limepanda nchini katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita baada ya vyama vya Jubilee na Kanu kutia saini mkataba wa muungano.

Hatua hiyo ilichangia mabadiliko ya uongozi wa mrengo wa wengi katika Seneti.

Waliopokonywa nyadhifa zao za uongozi ni maseneta wandani wa Naibu Rais William Ruto, wakiwemo Kipchumba Murkomen, Susan Kihika na Kithure Kindiki kutoka nyadhifa za Kiongozi wa Wengi, Kiranja wa Wengi, na Naibu Spika, mtawalia.

Muungano wa KCCB umewataka wanasiasa kuelekeza juhudi zao katika vita dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona na mpango wa kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko na maporomoko ya ardhi.

“Huu ni wakati mwafaka wa viongozi wetu kuungana kukabiliana na changamoto zinazowakabili Wakenya. Ikiwa hatutazima Covid-19 hakutakuwa na watu ambao watashiriki uchaguzi mkuu mnamo 2022,” akasema Askofu Mengich kwa niaba ya maaskofu wenzake, wanachama wa KCCB.