Maaskofu wafunguka kuhusu corona Tanzania, wataka wananchi waambiwe ukweli

Maaskofu wafunguka kuhusu corona Tanzania, wataka wananchi waambiwe ukweli

LOUIS KALUMBIA NA MASHIRIKA

Viongozi wa makanisa nchini Tanzania sasa wanataka waumini wapewe habari sahihi kuhusu maambukizi ya corona nchini humo.

Kanisa la Evangelical Lutheran Church of Tanzania (ELCT) limewaagiza viongozi wake kuwapa waumini habari za kweli kuhusu jinsi ya kujikinga na kuzuia msambao wa virusi hivyo.

Hatua ya kanisa hilo inajiri siku mbili baada ya kanisa katoliki nchini humo kuitaka serikali kueleza raia habari sahihi kuhusu ugonjwa huo.

Kwenye barua kwa maaskofu wa dayosisi na wanachama wa baraza la kitaifa mkuu wa kanisa la ELCT, Askofu Dkt Fredrick Shoo, anasema ripoti zinaonyesha wazi kuwa Covid 19 inasambaa kote ulimwenguni huku aina mpya zikizuka inavyoshuhudiwa katika nchi kama Uingereza.

Anasema Tanzania, ikiwa sehemu ya ulimwengu, haiwezi kujitenga kutoka mataifa mengine.

“Kwa hivyo, wale ambao miongoni mwetu tumepatiwa majukumu ya kuongoza watu wa Mungu, tunawajibu kwa kuwapa watu wetu maarifa na habari za kweli,” anasema na kuongeza: “Kupitia barua hii, ninataka kuwaambia, kupitia umoja wetu tuendelee kuwahimiza waumini na jamii kwa jumla kwamba licha ya maombi na kumtegemea Mungu, hatufai kupuuza onyo la wataalamu wa afya.”

“Ni jukumu letu kuwa waangalifu. Haikiuki imani yetu, wala sio dhambi au kosa la uhalifu; mbali ni kujaribu Mungu kwa kukataa onyo,” alisema Askofu Shoo na kuwakumbusha jinsi Yesu Kristo alivyojaribiwa na shetani nyikani.

Katika waraka wake, anawaonya viongozi wa makanisa waepuke kujaribu Mungu kuhusu corona akisema kupitia kitabu cha Hosea 4:6 Mungui anasema “watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima.”

Anasema kwamba ugonjwa huo ulipozuka mwaka jana uliharibu mifumo yote ya maisha ulimwenguni.

“Licha ya hatua zote, athari zake hazikuweza kuepukwa. Kanisa liliomba likizingatia tahadhari. Tunashukuru kwamba kanisa na watu wa imani nyingine waliendelea kukutana katika maeneo tofauti ya ibada kuabudu Mungu,” anaeleza.

Siku aliyoandika barua hiyo, Rais wa muungano wa maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Gervas Nyaisonga aliwaagiza wakuu wa makanisa kuweka hatua za kuzuia kusambaa kwa corona.

Imeibuka kuwa asasi za serikali sasa zinaagiza wafanyakazi kuzingatia kanuni za kujikinga wasiambukizwe virusi hivyo.

Tanzania iliyo na watu 60 milioni ilijitenga na ulimwengu kuanzia Aprili mwaka jana ilipoacha kutangaza idadi ya maambukizi ya virusi hivyo. Wakati huo ilikuwa imeripoti visa 509.

Baadhi ya maafisa wa afya waliokosoa msimamo wa Rais John Magufuli kuhusu corona walifutwa kazi.

Serikali ilivumisha utalii wa kimataifa katika juhudi za kuepuka uchumi kuathirika kama nchi jirani zilizotangaza hatua kali ikiwemo kafyu.

You can share this post!

Raila atetea Uhuru kuhusu mapungufu ya Jubilee

Wakazi wafurahia corona kupunguza ulevi vijijini