Maaskofu wahimiza serikali ikarabati daraja la mto Enziu

Maaskofu wahimiza serikali ikarabati daraja la mto Enziu

Na PIUS MAUNDU

WITO unaendelea kutolewa daraja la mto Enziu ambako basi lilianguka na kuporomoka majuma mawili yaliyopita kisha kusababisha maafa ya watu 32, likarabitiwe ili kuzuia majanga mengine siku zijazo.

Mnamo Jumamosi, ndugu wawili ambao ni waumini wa kanisa hilo, Stephen Kang’ethe na Kenneth Wanzala Okinda, waliokuwa kati ya walioangamia, walizikwa katika makaburi ya kanisa hilo.Marehemu Okinda na Kang’ethe walizikwa kulingana na itikadi ya kanisa Katoliki kwenye makaburi ya Kaumuni hafla iliyoongozwa na Maaskofu Joseph Mwongela na Norman King’oo ambao ni wakuu wa Dayosisi ya Kitui na Machakos mtawalia.

Bw Kang’ethe alikuwa dereva wa basi hilo la kanisa lililokuwa likiwasafirisha wanakwaya wa Muithi Museo Mwingi, kuhudhuria hafla ya harusi katika mji mdogo wa Nuu. Naye Bw Okinda alikuwa mshauri wa kanisa hilo kuhusu masuala ya elimu akitekeleza majukumu hayo kwa ustadi mno.

Waombolezaji waliwamiminia wawili hao sifa tele wakiwataja kama vielelezo bora kupitia huduma walizotoa kanisani. Aidha walitajwa kama waliojikita zaidi katika kusambaza injili na kuwafikia wengi kwenye kazi ya utumishi wa Mungu.

Nalo kanisa liliwashukuru wazazi wa wawili hao kwa kuwaruhusu walitumikie wakati wa uhai wao. Ingawa hakuna mwanasiasa ambaye alihudhuria mazishi hayo wikendi, Maaskofu King’oo na Mwongola, walikashifu serikali kwa kutofanya lolote kukarabati daraja hilo kabla na baada ya tukio hilo.

Maaskofu hao walisema kuwa si daraja hilo pekee bali hata nyanja nyingine za maendeleo zimetelekezwa na utawala wa Jubilee.“Mto ambako watu hawa walifariki unafaa kuwa na daraja. Maendeleo halisi yanazingatia na kuheshimu maisha ya watu.

Si lazima uwe tajiri ndipo uhudumiwe na serikali,“Inasikitisha kuwa tulisafiri kilomita kadhaa kwa kupitia mji wa Machakos ilhali Kitui ni karibu sana na Makueni. Wakazi wa Ukambani wanafaa waletewe miradi ya maendeleo kama tu Wakenya wengine,” akasema Askofu Mwongela.

Kufuatia tukio hilo, Katibu katika wizara ya Uchukuzi anayesimamia miundomsingi, Bw Paul Maringa, aliahidi kuwa serikali itajenga daraja la mto Enziu kwa kima cha Sh600 milioni kuanzia mwezi ujao.Aidha kigogo wa siasa za Ukambani Kalonzo Musyoka, Gavana wa Kitui Charity Ngilu na mbunge wa Mwingi ya Kati Gideon Mulyungi kwenye hafla mbalimbali siku za nyuma, wameahidi kuhakikisha ujenzi huo unaendeshwa ili kuzuia ajali nyingi.

Hata hivyo, maaskofu hao waliwataka wakazi wa Ukambani wawachague viongozi wanaojali maslahi yao wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 badala ya wale wanaowasahau baada ya kutwaa nafasi za uongozi.“Si vyema enzi hizi viongozi kulazimshwa kukumbatia miradi baada ya janga kutokea.

Kwa hivyo, yafaa tuwachague viongozi ambao wanazingatia sana maslahi ya raia kwa kuwapa miradi ya maendeleo,” akasema Bw King’oo.

You can share this post!

Raga: Kabras, Oilers juu ligi ikienda Krisi

Koome na idara yake kuwa na kibarua kikubwa mwaka ujao

T L