Michezo

Mabadiliko kikosini Simbas duru za Dubai na Cape Town zikinukia

November 22nd, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Mkuu wa timu ya Kenya Sevens, Paul Murunga, amefanya mabadiliko sita ikiwemo kujumuisha sura mpya Daniel Taabu, Johnston Olindi na Brian Wahinya katika kikosi kitakachowania ubingwa wa duru mbili za ufunguzi za Raga ya Dunia msimu 2018-2019 katika miji ya Dubai (Milki za Kiarabu) na Cape Town (Afrika Kusini).

Taabu, Leonard Mugaisi, Alvin Otieno, Wahinya, Cyprian Kuto, Charles Omondi na aliyekuwa nahodha Herman Humwa pekee ndio wamesalia kutoka kikosi kilichoshinda medali ya fedha katika Kombe la Afrika mjini Monastir, Tunisia mwezi Oktoba.

Eliakim Kichoi, Michael Wanjala, Derrick Keyoga, Benjamin Marshall na Gramwel Bunyasi ambao walikuwa Monastir hawajapata namba katika kikosi cha Murunga kitakachoshindania taji la Dubai mnamo Novemba 30 na Desemba na ubingwa wa Cape Town mnamo Desemba 8-9.

Nafasi zao zimetwaliwa na Dennis Ombachi, Eden Agero, Eric Ombasa, Samuel Motari na Jeffery Oluoch, ambaye aling’aa sana msimu 2017-2018, na Olindi.

Agero, Humwa, Otieno, Olindi, Taabu, Omondi, Ombachi, Kuto na Mugaisi walikuwa katika timu ya Shujaa iliyokamilisha mashindano ya Safari Sevens katika nafasi ya pili nyuma ya Samurai majuma machache yaliyopita uwanjani RFUEA jijini Nairobi. Nao Motari, Wahinya na Ombasa walikamilisha Safari Sevens katika nafasi ya tatu wakiwa katika timu ya Morans.

Taabu na Olindi waling’ara sana wakati wa mashindano ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande yaliyokamilika mwezi Septemba. Otieno na Motari walikuwa katika kikosi cha Shujaa kilichoandikisha historia kwa kushinda duru katika Raga ya Dunia wakati Kenya ilitwaa taji la Singapore Sevens mwaka 2016.

Wanarejea katika Raga ya Dunia baada ya kuwa nje kwa muda mrefu sawa na Omondi, Kuto na Mugaisi ambao walipeperusha bendera ya Kenya katika mashindano haya ya kifahari mara ya mwisho mwaka 2015. Ombachi, Agero, Ombasa, Humwa na Oluoch walishiriki Raga ya Dunia msimu uliopita.

Mfungaji wa zamani wa miguso migi duniani katika Raga ya Dunia Collins Injera anaongoza orodha ya wachezaji nyota watakaokosa ziara ya Dubai na Cape Town.

Injera pamoja na Samuel Oliech, Andrew Amonde, William Ambaka na Nelson Oyoo wako nchini Ufaransa kwa mchujo wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande utakaokamilika Novemba 23, 2018. Wachezaji kama Billy Odhiambo, Daniel Sikuta, Brian Tanga, Arthur Owira, Frank Wanyama na Oscar Ayodi ambaye alikuwa nahodha wa Kenya kwa kipindi kikubwa msimu uliopita, hawako kikosini.

Duru za Dubai na Cape Town zitakuwa mtihani mzuri kwa Kenya kuona kama inapiga hatua mbele katika kuunda kikosi kipya ama bado inahitaji wachezaji wengi walio na uzoefu ambao imewacha nje. Mjini Dubai, Shujaa imetiwa katika Kundi B pamoja na Fiji, Scotland na Ufaransa mbazo huibabaisha sana.

Miamba Fiji pia wametangaza kikosi chao. Kocha Gareth Baber atakosa huduma za Paula Dranisinikula na Josua Vakurunabili, ambao wanauguza majeraha.

Shujaa: Dennis Ombachi (Nondies), Alvin Otieno (Homeboyz), Charles Omondi (Homeboyz), Leonard Mugaisi (Homeboyz), Eden Agero (Nahodha/Kenya Harlequin), Eric Ombasa (Menengai Oilers), Samuel Motari (Impala Saracens), Herman Humwa (Kenya Harlequins), Jeffery Oluoch (Homeboyz), Daniel Taabu (Mwamba), Brian Wahinya (Blak Blad), Johnston Olindi (Homeboyz) na Cyprian Kuto (Homeboyz).

Fiji: Mesulame Kunavula, Kalione Nasoko, Apenisa Cakabalvu, Beniamino Vota, Sevouloni Mocenecagi, Ratu Meli Derelagi, Jerry Tuwai, Waisea Nacugu, Vatemo Ravouvou, Aminoni Nasilasila, Vilimone Botitu, Alosio Naduva na Filimoni Tuimaba.