Habari

Mabaki ya Wakenya walioangamia katika ajali ya ndege Ethiopia yaletwa

October 14th, 2019 2 min read

Na JAMES KAHONGEH, ERIC MATARA na PHYLIS MUSASIA

MABAKI ya Wakenya 28 kati ya 32 walioangamia Machi 10, 2019 katika ajali ya ndege ya Ethiopia yameletwa; familia zilizofiwa zafanya ibada JKIA

Majeneza maalumu yaliyobeba mabaki hayo yamesafirishwa kwa ndege ya shirika la Ethiopian Airlines iliyotua Jumatatu katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) dakika chache kabla ya saa nne za asubuhi.

Familia na marafiki za wahanga wa ajali hiyo walijumuika katika eneo la watu mashuhuri (VIP) katika uwanja huo ambapo wamepewa ushauri nasaha.

Ni watu wa karibu wa familia ndio wanapewa mabaki hayo ya wapendwa wao.

Kwa muda wa miezi saba tangu ilipotokea ajali hiyo eneo la Bishoftu, Ethiopia ambapo watu wote 157 waliokuwa kwa ndege ya Boeing 737 MAX , familia zilikuwa bado kuzika mabaki ya wapendwa wao.

Maafisa wa Ethiopia walisema miili iliteketea kiasi cha kutotambulika ambapo hata vipimo vya vinasaba, DNA, vilichukua muda wa zaidi ya siku 240 kubainishwa wazi.

Ndege hiyo iliyokuwa ikielekea Nairobi ilianguka katika eneo la Bishoftu, Ethiopia, dakika chache baada ya kuondoka katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Bole, Addis Ababa.

Jumapili, familia ya Bw John Quindos Karanja ambayo ilipoteza jamaa wao watano, ilisema wanapanga kusafirisha mabaki ya miili ya jamaa zao kwa mazishi Alhamisi.

“Tunashukuru Wakenya wote kwa misaada waliyotolea familia yetu. Tutasafirisha mabaki ya wapendwa wetu baada ya kutambuliwa. Tunapanga kuwazika Alhamisi, Oktoba 17,” ikasema taarifa kutoka kwa Bw Karanja ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo.

Bw Karanja, 61, ambaye ni mwalimu mstaafu, alipoteza jamaa zake watano wakiwemo mke wake Ann Wangui Karanja, bintiye Caroline Karanja na wajukuu watatu ambao ni Ryan Njoroge aliyekumbana na mauti akiwa na umri wa miaka saba, Kellie Wanjiku akiwa na umri wa miaka mitano, na Rubi Wangui (miezi tisa wakati mauti yanamkumba).

Jamaa wa familia nyingine kutoka Kipkelion ambayo pia ilipoteza mpendwa wao Cosmas Kipng’etich Rogony kwenye mkasa huo, pia walithibitisha kwamba baadhi yao walisafiri kwenda kuchukua mabaki ya mwili wake ili kuleta nyumbani kwa mazishi.

“Familia ya marehemu Rogony ilisafiri na wanatarajiwa kurejea kesho,” akasema jamaa wa familia hiyo.

Rogony ambaye alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya General Electric kitengo cha afya, aliacha binti mwenye umri wa mwaka mmoja na mjane Bi Miriam Wanja mwenye umri wa miaka 27.

Nyumbani kwao ni kijijini Saoset, Kaunti Ndogo ya Kipkelion Magharibi.

Mnamo Machi, familia hizo ziliandaa misa kuashiria msiba na maombi ingawa hapakuwa na miili yoyote kwenye majeneza yaliyotumiwa.

Imechukua zaidi ya miezi saba kwa ripoti ya DNA kuhusu waliofariki kutolewa, na kuruhusu familia kuandaa mazishi inavyostahili kwa wale ambao sehemu za miili yao zilipatikana.

Kufikia sasa, kuna baadhi ya Wakenya ambao wameungana kwenye kesi inayotaka kampuni ya utengenezaji ndege ya Boeing kulipa ridhaa ya Sh100 bilioni.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mahakama ya Amerika na kampuni kubwa za uwakili nchini humo.

Familia hizo zimeuliza kwa nini ndege aina ya Boing 737 MAX 8 hazikupigwa marufuku ilhali kulikuwa na ajali nyingine awali iliyohusisha aina hiyo ya ndege kutoka Indonesia ambapo wasafiri wote 189 waliokuwemo waliangamia.

Hivi majuzi, Boeing ilitangaza kwamba familia zilizoathirika katika mkasa huo zitalipwa Sh15 milioni kila moja.