Michezo

MABAO EPL: Arsenal watoka nyuma na kuzamisha matumaini ya mabingwa Liverpool kuvunja rekodi ya Manchester City

July 16th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya Liverpool ya kuweka rekodi mpya ya kuwa kikosi kilichojizolea pointi nyingi zaidi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) yalizimwa na Arsenal uwanjani Emirates kwa kichapo cha 2-1 mnamo Julai 15, 2020.

Sadio Mane aliwaweka Liverpool kifua mbele kunako dakika ya 19 kabla ya Alexandre Lacazette kusawazisha mambo katika dakika ya 32. Lacazette alichangia pia bao la pili la Arsenal lililofumwa wavuni na chipukizi Reiss Nelson. Goli la kwanza la Arsenal lilikuwa zao la masihara ya beki Virgil van Dijk huku la pili likitokana na utepetevu wa kipa Alisson Becker.

Kichapo hicho kilikuwa cha tatu kwa Liverpool ambao ni mabingwa wapya wa EPL kupokezwa hadi kufikia sasa katika kampeni za msimu huu.

Tangu chombo chao kizamishwe na Watford kwa mabao 3-0 mnamo Februari 29, 2020 uwanjani Vicarage Road, Liverpool walibebeshwa tena mzigo wa mabao 4-0 na Manchester City mnamo Julai 2 uwanjani Etihad.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool kwa sasa watapokezwa rasmi kombe la EPL msimu huu mnamo Jumatano ijayo ya Julai 22 wakati wa gozi litakalowakutanisha na Chelsea uwanjani Anfield.

Baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Burnley uwanjani Anfield mnamo Julai 11, Liverpool walihitaji kuwapepeta Arsenal na kusajili ushindi katika mechi mbili za mwisho wa msimu huu dhidi ya Chelsea na Newcastle United ili kuivunja rekodi ya pointi 100 iliyowekwa na Man-City waliotawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza chini ya kocha Pep Guardiola mnamo 2017-18.

Katika msimu wa 2018-19, Man-City walihifadhi ufalme wa taji la EPL kwa alama 98, moja pekee mbele ya Liverpool walioridhika na nafasi ya pili.

Kwa sasa, masogora hao wa Klopp wanajivunia alama 93 huku pengo la pointi 18 likitamalaki kati yao na Man-City ambao ni nambari mbili jedwalini. Ina maana kuwa Liverpool wana uwezo wa kufikisha jumla ya alama 99 pekee msimu huu iwapo watawaangusha Chelsea na Newcastle katika mechi zao zilizosalia ligini.

Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama 53, sita nyuma ya Leicester City na Manchester United. Huku wawili hao wakipigania nafasi ya kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, Arsenal wangali na matumaini finyu ya kuingia ndani ya mduara wa sita-bora na kufuzu moja kwa moja kwa kivumbi cha Europa League.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Aprili 2015 kwa Arsenal kuwabwaga Liverpool katika EPL na mara ya kwanza kwa kocha Jurgen Klopp kupoteza mechi ya EPL dhidi ya Arsenal baada ya kuibuka na ushindi mara tano na kuambulia sare mara tatu katka jumla ya michuano minane iliyopita.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Man-City katika nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Julai 18 uwanjani Wembley, Uingereza kabla ya kushuka dimbani kukwaruzana na Aston Villa na Watford katika mechi mbili za mwisho za EPL msimu huu.

MATOKEO YA EPL (Julai 15, 2020):

Burnley 1-1 Wolves

Man-City 2-1 Bournemouth

Newcastle 1-3 Tottenham

Arsenal 2-1 Liverpool