Michezo

Mabao ya Fernandes na Cavani yapunguza joto na presha kambini mwa Mancheter United

November 7th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BRUNO Fernandes alifunga mabao mawili na kusaidia Manchester United kutoka nyuma na kuwapepeta Everton 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha ugani Goodison Park mnamo Novemba 7, 2020.

Bernard Duarte aliwaweka Everton kifua mbele kunako dakika ya 19 baada ya kumwacha hoi beki Aaron Wan-Bissaka kabla ya Fernandes kuwarejesha Man-United mchezoni kunako dakika ya 25.

Goli la Fernandes aliyeridhisha zaidi katika mechi hiyo iliwapa Man-United motisha ya kuendeleza mashambulizi kwenye lango la wenyeji wao na juhudi zake zikazaa matunda kwa mara nyingine katika dakika ya 32 alipowafungia waajiri wake bao la pili.

Sajili mpya Edinson Cavani aliwafungia Man-United goli la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili sekunde chache baada ya fowadi Lucas Digne wa Everton kushuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli la kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Licha ya ushindi, Man-United wanasalia miongoni mwa vikosi vilivyopo katika nafasi 10 za chini jedwalini huku Everton wakisalia katika nafasi ya tano baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo.