Michezo

Mabao ya Rashford yazamisha Chelsea

November 1st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MANCHESTER ilifuzu kwa robo-fainali ya michuano ya Carabao Cup kutokana na frikiki ya Marcus Rashford aliyekuwa pia mfungaji wa bao la kwanza katika ushindi wao wa 2-1 dhidi ya wenyeji Chelsea, ugani Stamford Bridge.

Mshambuliaji huyu wa timu ya taifa ya Uingereza alikuwa ameifungia timu yake bao la kwanza kutokana na mkwaju wa penalti iliyopeanwa baada ya beki wa kushoto Marcos Alonso kumchezea ngware Daniel James.

Michy Batshuayi aliisawazishia Chelsea ambao walikuwa wakijivunia ushindi wa awali wa mechi saba kutokana na kombora la nje ya kijisanduku cha eneo la hatari, kabla ya Rashford kumimina wavuni bao la ushindi kutokana na kombora la umbali wa mita 30.

“Binafsi, nilimuona Rashford akicheza kama Cristiano Ronaldo,” alisema Solskjaer. “Kijana alipiga penalti kwa ujasiri mkubwa na kutufungia bao la pili ambalo lilitupa ushindi huu muhimu. Nampa heko.

“Daima anapenda kufanya mazoezi ya kupiga penalti. Kazi yangu imekuwa kumuonyesha jinsi anavyweza kufunga mabao akiwa ndani ya kijisanduku. Mara kwa mara amekuwa akitufungia mabao muhimu.”

Katika mechi hiyo, kocha Solskjaer alipanga kikosi kikali kuliko mpinzani wake Frank Lampard ambaye aliamua kuwapa nafasi makinda kuonyesha uwezo wao, huku miamba kadhaa wakibakia nje. Ni Brandon Williams pekee aliyekuwa mgeni katika kikosi hicho cha Manchester United.

Uamuzi wake ulizaa matunda, kwa kukiwezesha kikosi chake kuandikisha ushindi wa tatu mfululizo, mechi zote zikiwa za ugenini baada ya kwenda mechi sita bila ushindi.

Awali kwenye mechi hiyo, Scott McTominay alikaribia kufunga bao kabla ya Rashford kufunga penalti ambayo ilimsumbua kipa Willy Caballero wa Chelsea.

Mabadiliko kikosini

Kwa upande mwingine, Chelsea walifanya mabadiliko sita katika kikosi kilichoshinda Burnley 4-2 mwishoni mwa wiki.

Lakini hata Christian Pulisic aliyeonyesha kiwango cha juu cha mchezo siku hiyo na kufunga mabao matatu, alishindwa kuwika mbele ya Manchester United.

Batshuayi alisawazisha baada ya kuchomoka na kumzidi maarifa beki tegemeo Harry Maguire kabla ya kuachilia kombora kutoka umbali wa yadi 25.

Baada ya mechi hiyo, kocha Frank Lampard wa Chelsea aliwaambia wanahabari kwamba timu yake haikupata nafasi za kufunga mapema, huku akiwapongeza vijana wake kwa kucheza mchezo wa kuvutia katika kipindi cha pili.